×

Ronaldo… Dakika Tisini Tu, Rekodi Kibao

TURIN, Italia: CRISTIANO Ronaldo ambaye ni mshindi mara tano wa Tuzo ya Ballon d’Or, wiki hii ameweka rekodi kadhaa ndani ya dakika tisini ambazo ni sawa na mchezo mmoja pekee kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

 

Staa huyo wa Juventus, alifanya hivyo wakati timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Bayer Leverkusen ukiwa ni mchezo wa Kundi D katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

 

Katika mchezo huo, Gonzalo Higuain, Federico Bernardeschi na Ronaldo ndiyo walifunga mabao wakati Juventus ikicheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Allianz.

Kupitia bao lake hilo na ushindi huo, Ronaldo aliweka rekodi kadhaa zifuatazo:-

 

BADO KINARA WA MABAO

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34, amezidi kujikita kileleni mwa wanao-ongoza kwa mabao kwenye michuano ya Ulaya ngazi ya klabu akifikisha mabao 128, juu ya Lionel Messi wa Barcelona mwenye mabao 112.

Ronaldo amefunga mabao hayo akiwa na timu tatu tofauti ambazo ni Manchester United mabao 15, Real Madrid (105) na Juventus (8), wakati Messi ameyafunga mabao yote akiwa na Barcelona pekee.

 

MWIBA KWA WAJERUMANI

Mpaka sasa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, hakuna mchezaji aliyefunga mabao mengi dhidi ya klabu kutoka nchi moja zaidi ya Ronaldo.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester United, ameshafunga mabao 27 katika mechi 25 dhidi ya timu za Ujerumani ambapo bao lake la 27 amewafunga Leverkusen.

 

AMKAMATA MESSI, RAUL

Ronaldo sasa ameshafunga katika misimu 14 mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya sawa na Raul na Messi.

Lakini pia kitendo cha kufunga bao dhidi ya Leverkusen, sasa inamaanisha Ronaldo yupo sawa na Raul kwa kuzifunga timu 33 tofauti kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

 

AVUNJA REKODI YA CASSILAS

Ronaldo sasa amevunja rekodi ya mchezaji wa zamani wa timu ya Real Madrid, Iker Casillas kutokana na kushinda mechi nyingi za Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ushindi wao dhidi ya Leverkusen, ni wa 102 kwa nyota huyo.