×

Kessy Awachoma Wakandarasi kwa JPM – Video

MBUNGE wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Kessy, amesema makandarasi wanashirikiana na baadhi ya watendaji na watumishi wilaya ya Nkasi kutafuna fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo akiongeza kwamba jambo hilo linasababisha miradi mingi kufa, mingine kutofanya kazi.

Mbunge huyo ametoa kauli hiyo leo Jumanne Oktoba 8, 2019 katika ziara ya Rais John Magufuli wilayani humo,  Mkoa wa Rukwa.

 

Katika ziara yake leo Magufuli amezindua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara ya Sumbawanga – Kanazi na kituo cha afya cha Namanyere.

 

Keissy amesema watumishi wa umma wanashirikiana na makandarasi kuiba fedha za umma na kutotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hasa huduma ya maji licha ya kulipwa fedha zao.

 

“Mheshimiwa Rais, Serikali yako inaleta fedha lakini makandarasi kwa kushirikiana na watumishi wako wanashirikiana kutuibia. Mkandarasi peke yake hawezi kuiba hela,  ni watumishi wako ndiyo wanawasaidia,” alisema Kessy.

 

Katika kujibu hoja za mbunge huyo, Rais Magufuli alisema:

“Nataka niwaambie kwa dhati kuwa Jimbo la Nkasi mna mbunge mzuri sana. Kessy anaongea ukweli na kuwatetea wananchi wake, anasema hadharani kuwa mkandarasi huyu hafai na angekuwa anapenda pesa na yeye angekatiwa chake akae kimya lakini anasema ukweli.

 

“Ingekuwa wabunge wanabadilishwa basi huyu Kessy ningempeleka akawe mbunge kule Chato, siyo kwamba Chato hawana mbunge mzuri kwa sasa, lakini ni vigumu kumpata mbunge kama huyu anayeweza kusimama na kusema hadharani matatizo yanayowakuta wananchi wake.”