×

SBL Yawekeza Bilioni 28.1 Kupanua Uzalishaji

Na Neema Adrian Kampuni inayoongoza kwa uzalishaji wa bia  ya Serengeti Breweries (SBL), imetangaza mpango wake wa upanuzi wenye thamani ya paundi milioni 10 (zaidi ya shilingi bilioni 28.1 za Kitanzania) kwa viwanda vyake vya Dar na Moshi.

Uwekezaji huo unapelekea kampuni hiyo kuongeza uwezo wake wa uzalishaji wa bia hivyo kukidhi mahitaji ya wateja wa bidhaa zake yanayoongeza kila siku.

Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Mark Ocitti amesema jijini Dar, leo kuwa, kazi ya upanuzi tayari imeanza Dar ambalo ni tawi la kwanza la uzalishaji kati ya matatu lililoanzishwa mwaka 1996. Matawi mengine ya uzalishaji ni Moshi na Mwanza.

“Upanuzi huu haumaanishi tu kupata uwezo wa ziada wa uzalishaji wa bia kwa sisi (SBL), lakini pia unaongeza fursa zaidi za ajira kwa Watanzania na kuongeza uhitaji zaidi wa shayiri, mahindi na mtama ambavyo kampuni hununua kutoka kwa wakulima wa ndani,” mkurugenzi mkuu huyo anasema.

SBL kwa sasa imeajiri wafanyikazi wa moja kwa moja zaidi ya 800 na wengine katika viwanda vyake. Kuna maelfu ya wanufaika wengine wakiwamo wasambazaji, wasafirishaji, wakulima, wamiliki wa baa na wafanyakazi ambao hutegemea bidhaa za kampuni hiyo kama chanzo cha mapato.

Kampuni hiyo hutegemea vyanzo vya ndani vya shayiri, mahindi na mtama kwa uzalishaji wake wa bia.

Mkurugenzi huyo anafafanua kuwa, hadi kufikia mwishoni wa mwaka jana, kampuni hiyo ilichukua nafaka za ndani hadi kufikia tani 15,000, ambayo ni sawa na asilimia 60 ya mahitaji kamili ya malighafi ya SBL kwa uzalishaji wa bia kwa mwaka.

SBL ina bidhaa nyingi zinazouzika na zina ubora wa hali juu kwa jina lake. Chapa yake kuu ya Serengeti Premium Lager imekuwa bia ya kwanza nchini Tanzania kufanywa kuwa malt kwa asilimia 100.

Hivi karibuni SBL ilizindua bidhaa yake nyingine ya Serengeti Premium Lite, ambayo ni ya kwanza nchini Tanzania iliyoingizwa sokoni mwaka wa 2017.

“Wateja wetu walionesha uhitaji wa bia halisi ya Kitanzania na ndiyo maana tulizindua Serengeti Premium Lite miaka miwili iliyopita. Watanzania wameipokea vyema bidhaa hii mpya ambayo imekuwa ikifanya vizuri katika soko,” amesema.

Utafiti uliofanywa na Kampuni ya Deloitte mwaka 2018 juu ya uchangiaji wa SBL kwenye uchumi wa Tanzania ulionesha kuwa, SBL ilichangia thamani ya shilingi bilioni 567 katika uchumi wa Tanzania kwa mwaka jana. Hii ni sawa na asilimia moja ya uchangia kwenye pato la taifa kwa bidhaa za ndani (GDP) ) ambalo kwa sasa linakadiriwa kufikia dola bilioni 55, karibia sawa na shilingi trilioni 127.