×

Umejiandikisha Kuchagua Viongozi? Soma Hapa…

Mtangazaji wa Global TV Online, Catherine Kahabi (kushoto) akizungumza na baadhi ya wananchi eneo la Buguruni-Chama jijini Dar es Salaam.
…Akiendelea kuzungumza na  wananchi wa  Buguruni.
Wananchi wakifunguka walivyojiandaa kuchagua viongozi.
…Akiwahoji kinanamama kupitia Global TV Online.
Mahojiano yakiendelea.

 

 

 

 

 

 

Harakati za kupiga kura zikiendelea. WAKATI zoezi la uandikishaji wa wananchi katika Daftari la Kudumu la Kupiga Kura kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu ukiendelea, baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam wameelezea walivyojipanga kuhakikisha hawaipotezi haki yao ya msingi.

 

 

Leo Jumatatu, mwandishi wetu alizunguka mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ili kuona mwamko wa wananchi katika zoezi hilo la kujiandikisha ambalo lilianza wiki iliyopita na linatarajiwa kufikia tamati Oktoba 17, mwaka huu baada ya kuongezwa siku tatu mbele. Awali ilitangazwa zoezi hilo kufikia tamati leo Jumatatu Oktoba 14, 2019.

 

Juma Abdallah ambaye ni mkazi wa Buguruni Malapa, alisema anashukuru kwa hatua nyingine imetimia ya kuchagua viongozi wapya wa serikali ambapo kwake anaona zoezi hilo linakwenda vizuri na amepanga kutofanya makosa.

 

 

“Nimejipanga kwenda kupiga kura, tayari nimejiandikisha, hivyo zoezi la upigaji kura likifika, nitawahi mapema kituoni kwani, sitafanya makosa katika kumchagua kiongozi nimtakaye ambaye ataleta maendeleo katika mtaa wangu,” alisema.

 

Naye Mama Abdul wa Mwananyamala, alisema kuwa, kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kujiandikisha mapema kimeonyesha mfano bora kwa raia, hivyo hana sababu za kubaki nyuma kuacha kufuata kile alichofanya Rais.

 

“Kupiga kura ni haki ya kila Mtanzania, hivyo sina sababu za kuipoteza haki yangu wakati Rais mwenyewe ameenda kujiandikisha, mimi ni nani hadi nibaki nyuma. Hapa nilipo nimeshajiandikisha, nasubiri siku ya kupiga kura niende kufanya uamuzi sahihi,” alisema Mama Abdul.

 

 

Wakazi wengine wa Dar es Salaam, walimpongeza Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jafo baada ya kutangaza kuongeza muda wa kujiandikisha kwani wengi wao walishindwa kujiandikisha mapema kutokana na changamoto ya mvua.

 

Wakazi hao pia waliushukuru uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam chini ya Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda kwa kutoa hamasa kwa wananchi ili wasikose haki yao ya msingi ya kuwapata viongozi wanaowataka.

 

Mbali na hilo, wakazi hao waliendelea kupaza sauti kwa kuwataka wenzao kama bado hawajajiandikisha, wafanye hivyo haraka ili kupata haki yao na kupuuzia maneno yaliyopo mtaani kwamba kujiandikisha sio lazima.