×

Vodacom Yamwaga Neema kwa Wanafunzi 7000 Tabora

KAMPUNI inayoongoza kwa teknolojia ya mawasiliano ya Vodacom kupitia taasisi yake ya Vodacom Tanzania Foundation leo imemwaga neema kwa kutoa msaada wa kompyuta na kipanga-njia (router) vilivyounganishwa katika intaneti kwa shule 14 za Wilaya ya Urambo, Tabora.

 

Msaada huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 67.6 ni sehemu ya mpango endelevu wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa taarifa muhimu katika sekta ya elimu.

Hii ni sehemu ya ushirikiano wa Vodacom na Mfuko wa Huduma za Mawasiliano (UCSAF) wa kutoa elimu shuleni kwa kutumia miundombinu bora ya teknolojia ya mawasiliano ya Vodacom.

 

Kupitia ushirikiano huo, jumla ya shule 300 na hasa zilizoko vijijini zitapata kompyuta zilizounganishwa na intaneti bure.

 

Akipokea msaada huo, katika shule ya Sekondari ya Urambo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, alisema msaada huo ni hatua muhimu kuelekea maendeleo ya teknolojia ya kidijitali.

“Maendeleo ya dijitali yanaonesha kuwapo mafanikio kutokana na uwepo wa kompyuta kama hizi katika shule zetu sambamba na kasi ya matumizi ya simu za mkononi nchini,” alisema Waziri Kamwelwe.

 

“Tunaamini kompyuta hizi ni hatua nyingine katika mchakato wa mabadiliko ya kidijitali. Tunawashukuru Vodacom Tanzania Foundation kwa msaada wao mzuri,” alisema Kamwelwe.

 

Naye Mkurugenzi wa Vodacom Foundation, Rosalynn Mworia alisema msaada huo ni sehemu ya ajenda ya Vodacom Foundation yenye lengo la kusaidia sekta ya elimu ili kutoa elimu bora na kuhakikisha wanafikia malengo ya milenia na ajenda ya kitaifa kama sehemu ya mradi wa shughuli za kijamii.

“Fursa za kidijitali ni nishati muhimu katika uchumi unaokua, zina matokeo ya haraka katika uchumi na jamii kwa jumla. Kwa pamoja zinachangia ukuaji wa uchumi, kuongeza mianya ya ajira pia ina mchango mkubwa katika kupunguza umaskini, huku ikitoa mwanya katika kuchochea ukuaji wa sekta muhimu kama vile elimu na afya,” alisema Mworia.

 

“Vodacom imeamua kuweka nguvu katika maendeleo kidigitali Tanzania. Ndiyo maana tunajivunia kutoa msaada huu leo ambao unajumuisha kompyuta, rota vyote vikiunganishwa katika mtandao vikiwa na thamani za zaidi ya shilingi milioni 67 katika shule 14 wilayani Urambo ambayo inategemea kuwafikia zaidi ya wanafunzi 7,000,” alisema Mworia.