×

CCM Yafuta Kura za Maoni, Uchaguzi Kurudiwa – Video

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka na kuweka wazi madai ya kuwapo rushwa katika kura za maoni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, huku kikiamuru kura hizo zirudiwe kwa baadhi ya maeneo yaliyoonekana kukiuka taratibu.

Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally amewaonya wanaojihusisha na vitendo hivyo na kusema vitendo hivyo na madai ya upendeleo ni dalili za kupanga safu kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao wa Rais, wabunge na madiwani, utakaofanyika 2020.

Dkt. Bashiru amesema malalamiko wanayoyapokea yanagusa uvunjifu wa kanuni kwa mtazamo wa rushwa au upendeleo au kupanga safu.

Katibu huyo alisema, kanuni za kuchuja wagombea hazikuzingatiwa kwenye baadhi ya maeneo na kwamba baadhi ya viongozi walichezea muhtasari kiasi cha kupishana kati ya Tawi, Kata na uamuzi wa Wilaya.

Alisema, kulikuwa na rafu za kuchomoa majina kwenye masanduku ya kura na masanduku kubomolewa na wengine wakitumia jina la Katibu Mkuu kuwa amewapa maelekeo ya kufanya wafanyayo.

Nyingine ni wasimamizi kuchelewa na kura za maoni zikaanza kupigwa baada ya saa tisa alasiri, na kwamba wagombea wote walioomba warudishwe kupigiwa kura.

Aidha, amesema “Marudio yanarekebisha uteuzi, kote uchaguzi urudiwe bila kuwachuja wapiga kura ili tuweke imani, ilikuwa tumalize Oktoba 29, tunaongeza siku mbili hadi Oktoba 31,” alisema Bashiru.