×

NBC Yaendelea Kuimarisha  Huduma za Kidigitali

Mkuu wa Kitengo cha Fedha Taslim na Miamala kwa wateja Wakubwa na wa Kati wa NBC, Jimmy Myalize akizungumza na baadhi ya wateja wao wa jijini Mwanza kuhusiana na huduma mbalimbali zitolewazo na benki yao.
…Jimmy Myalize akizungumza na baadhi ya wateja wao wa jijini Mwanza, Maleshi Mathade  kulia pamoja na Mitesh Metha.
…Jimmy Myalize akishikana mkono na mteja wa NBC kutoka Kampuni ya Marine Services, Erick Hamissi kwenye hafla hiyo.
Meneja wa Huduma kwa Wateja Wakubwa wa Benki ya NBC, Mary Opiyo wa tatu kushoto akishikana mikono na mteja wa benki hiyo, Mkurugenzi wa Bugando Medical Centre, Padre Englbert Nyandwi.

Mkuu wa Kitengo Cha Wafanyabiashra wa Kati wa NBC, Moses Minja kushoto akisalimiana na Erick Hamissi wa Kampuni ya Marine Services,  kwenye hafla hiyo.

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC), imeendelea kuongeza na kuimarisha huduma zake za kibenki kwa njia za kidigitali ili kuwawezesha wafanyabiashara na wateja wengine kufanya miamala mingi  ya kibenki mahali walipo imeelezwa jijini Mwanza hivi karibuni.

 

Akizungumza na wateja wa benki hiyo jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya mwezi wa huduma kwa wateja wa NBC, Meneja  Huduma katika  Kitengo cha Wateja wa Makampuni wa benki hiyo, Mary Opiyo alisema benki hiyo imerahisisha huduma zake nyingi kwenda  kidigitali ili kuwafanya wateja wao kupata muda zaidi wa kufanya biashara zao kuliko kupata huduma hizo katika matawi yao.

 

“Sasa mteja wetu anaweza kufanya malipo akiwa ofisini kwake kwa njia ya mtandao wa intaneti akatuma pesa kwa wateja wake ambao pengine ingebidi awapelekee au waje pale, NBC itaendelea kuboresha na pia imo mbioni  kuongeza huduma nyingine bora zaidi hususan malipo kwa njia ya mtandao ili kutengeneza fursa mbalimbali za kibiashara kwa wateja wetu”, aliongeza meneja huyo.

 

Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Kitengo cha Fedha Taslimu na Miamala kwa wateja Wakubwa na wa Kati wa beni hiyo, Jimmy Myalize alisema  mkutano huo una lengo la kuwashukuru wateja wao  kwa biashara wanayowapa na kuweza kuwaamini wakawa benki  waitumiayo  kwa ajili ya mambo yao ya kifedha.

 

Alisema pia katika kukutana kwao wameweza  kuwafahamisha bidhaa zao mpya,  benki ipo wapi na maendeleo ya benki kwa ujumla na pia kupata mrejesho kutoka kwao juu ya huduma za NBC na kama kuna maeneo wangependa yaboreshwe ili kuweza kuwahudumia vizuri zaidi.

 

“Pia tunawakutanisha wateja wetu ili kuweza kuongea biashara na  kutengeneza  fursa za kibiashara kati yao jambo litakalosaidia wateja wetu kukua kibiashara kwani mteja anapokua na sisi kama benki tunakua”

 

 

Benki ya NBC huadhimisha Mwezi wa Huduma kwa Wateja mwezi wa Oktoba kila mwaka kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii kama vile kutoa misaada mbalimbali na kutoa elimu ya kifedha na ujasiriamali kwa makundi tofauti, kutembelea wateja wao mahali walipo  na  kufanya mikutano na wateja hao.