
VIJANA ambao ni wafuasi na wakereketwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamemchukulia fomu Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Alikaeli Mbowe, ili kumshawishi agombee uenyekiti wa chama hicho na kuendelea kutetea kiti chake.
Tukio hilo limetokea leo Novemba 25, 2019 katika Ofisi za Chadema, Wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, baada ya vijana hao kuchukua fomu.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo, Daniel Ngogo, aliyeratibu zoezi hilo, amesema wamefanya hivyo wakiamini kwamba, Mbowe atawavusha salama katika siasa za sasa.
“Tumechangisha fedha kwa watu wa kawaida. Mpaka jana tumepata Mil 5.6. Tunatambua fomu ni Sh. 1 milioni, lakini tulikuwa hatuna mfumo wa kuzuia watu kuchangia.
“Tumeshalipia fomu. Itakayobaki tunamkabidhi mwenyewe,” amesema Ngogo akiongeza kwamba watamkabidhi Mbowe fomu hiyo, siku ya Jumatano, Novemba 27, mwaka huu.