×

Wachungaji, Mashekhe Wawachapa Viongozi Mwanza

TIMU ya soka ya viongozi wa serikali ya mkoa wa Mwanza wakiongozwa na Katibu Tawala wa mkoa huo, Christopher Derek Kadio, imejikuta katika wakati mgumu baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa viongozi wa asasi za kidini wakiwemo wachungaji na mashehe  katika mchezo wa kirafiki  uliopigwa Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Mchezo huo uliopigwa jana Ijumaa ulikuwa na lengo la kuleta umoja na  mshikamano kwa wana-Mwanza kuelekea maadhimisho ya miaka 58 tangu Tanzania Bara ipate uhuru wake ambapo maadhimisho yake kitaifa yatafanyika Desemba 9 mwaka huu jijini humo.

Akizungumza na www.globalpublishers.co.tz, Kadio ambaye aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella,   alisema sababu ya kupoteza mchezo huo ni kutokana na wachezaji kutofanya mazoezi kwa kubanwa na shughuli nyingi za kiserikali.

“Timu yangu imepoteza mchezo huo kwa kuwa wachezaji wangu hawapati muda wa kufanya mazoezi mara kwa mara kutokana na kubanwa na majukumu, naamini  mchezo ujao tutafanya vizuri zaidi,” alisema .

Naye kocha mkuu wa timu ya wachungaji na mashekhe waliowakilisha asasi za kidini mkoani hapa, Dkt. Jacob Mutash, ambaye ni mchungaji wa kanisa la EAGT Kiloleli jijini hapa, amesema siri kubwa iliyowapa ushindi ni maombi.

“Kabla ya kuanza kwa mchezo huo kwa imani zetu,  Wakristo walisali pia mashekhe nao walisali kwa ajili ya mchezo huo na Mungu ametubariki tumepata ushindi wa mabao 3-1,  hiyo ni baraka na wao wameshindwa kupata matokeo pengine kwa kuwa hawakumuomba Mungu,” alisema

Kivutio kikubwa katika mchezo huo alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba , ambaye alivunja rekodi kwa kutoka na kuingia uwanjani kwa mara tatu mfululizo hasa baada ya kuona timu yake imezidiwa lakini pia aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Taifa, Mohamed Kiganja, ambapo naye alishiriki katika mchezo huo kwa kuichezea timu ya viongozi wa serikali ya Mkoa wa Mwanza.

Na Johnson James – GPL MWANZA

Leave a Comment