
MBEYA: Dunia katili! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia baba aliyejulikana kwa jina la Lubisi Mwakalundwa (62), mkazi wa Kijiji cha Nkunga Kata ya Nkunga Wilaya ya Rungwe jijini Mbeya, kudaiwa kuuawa kikatili na kifo chake kuacha simanzi kubwa.
Akizungumza na Gazeti la kwa huzuni na masikitiko makubwa, dada wa marehemu, Tujeko Lubisi alisema mke wa marehemu, baada ya kugundua mumewe amechelewa kurudi nyumbani, alifuatilia njia ya shambani na kukuta panga la marehemu limetapakaa damu na pembeni kuna mwili wa marehemu ukiwa kwenye kiroba kilichoshonwa kwa kamba ya katani.
Alisema kuwa, baada ya hapo aliwaita majirani na kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Nkunga, Mariam Nurdin aliyefika eneo hilo na kukuta mwili ukiwa kwenye kiroba kisha akaita Polisi ambao waliuchukua hadi Hospitali ya Makandana- Rungwe kwa ajili ya uchunguzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, ACP Ulrich Matei alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kwamba tayari Jeshi la Polisi mkoani humo linawashikilia watu watu kwa tuhuma za mauaji hayo.
Kamanda Matei alisema kuwa, watuhumiwa hao walidai kuwa marehemu alikuwa akiwasumbua kwa uchawi aliodaiwa kuupata nchi jirani ya Malawi.
Kamanda Matei alisema tukio hilo la mauaji lilitekelezwa na watu hao Desemba 3, mwaka huu, muda wa jioni, mita chache kutoka nyumbani kwa marehemu alipotoka shambani.
Baada ya uchunguzi kufanyika, Kamanda Matei alisema mwili wa marehemu ulikutwa umekatwa kisogoni na vitu vyenye ncha kali na majeraha mikononi na miguuni ambapo mwili ulikabidhiwa kwa ndugu na mazishi kufanyika Desemba 5, mwaka huu nje ya nyumba ya marehemu.
Kamanda huyo wa polisi alisema watuhumiwa wanahojiwa na uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Aidha, aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na pia watu wanaojihusisha na imani za kishirikina waache kwani vitendo hivyo havileti amani katika jamii.
Kwa upande wake, mtoto wa marehemu, Sunday John alisema alipata taarifa za kifo cha baba yake kutoka kwa mama yake mdogo na kwamba baba yake hakuwa na ugomvi na mtu yeyote.
Naye Diwani wa Kata ya Nkunga, Zebedayo Mwasanganga alisema kitendo kilichofanywa na wauaji hao si cha kiungwana kwani kinaleta hofu katika jamii na kwamba wananchi watoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kuwabaini wahusika wa mauaji.
Stori: Ezekiel Kamanga