×

Ozil Aiponza Arsenal, Wachina Wamvaa

SHIRIKA la Habari la China (CCTV) jana Jumapili lilifutilia mbali mpango wa kuonyesha mechi ya kati ya timu ya Arsenal na Manchester City kufuatia matamshi ya kiungo wa kati wa Arsenal, Mesut Ozil, ambaye alichapisha katika mitandao ya kijamii kuhusu jinsi Waislamu wa Uighurs wanavyoteswa nchini China.

 

Arsenal ilikanusha kutokana na matamshi ya mchezaji wake huyo raia wa Ujerumani ikisema kuwa yenyewe kama klabu haijihusishi na masuala ya kisiasa na kwamba hayo ni maoni kibinafsi ya Ozil.

 

Taarifa hiyo ya Gunners ilichapishwa katika mtandao wa Weibo nchini China ambapo Gazeti la The Global Times lilitaja matamshi ya Ozil kuwa ya ‘kusikitisha’ na kuongezea kuwa shirikisho la soka nchini China lilisema kwamba matamshi ya Ozil ‘hayakubaliki’ na yameumiza hisia za watu wengi China.

 

CCTV iliahirisha kuonyesha mechi hiyo na badala yake ikaonyesha mechi kati ya Tottenham dhidi ya Wolves.

 

Makundi ya haki za kibinadamu yanasema kwamba karibu watu milioni moja, wengi wao kutoka kwa jamii ya Uighur waliko  Waislamu wengi, wanadaiwa kukamatwa bila kufunguliwa mshtaka katika kambi moja ya jela, lakini China imesema kwamba Waislamu hao wanapatiwa mafunzo katika kambi ili kukabiliana na ghasia na itikadi kali za kidini.

 

Katika chapisho lake,  Ozil ambaye ni Muislamu aliwaita Uighurs ”mashujaa ambao wanapinga mateso” na kuikosoa China pamoja na idadi kubwa ya Waislamu waliolifumbia macho jambo hilo. China mara kwa mara imepinga kwamba inawatesa Waislamu wa jamii ya Uighurs katika taifa hilo.

 

Mwezi Oktoba, shirikisho la mpira wa vikapu nchini Marekani lilikumbwa na hasara kubwa ya kifedha baada ya tamko la mtandaoni kutoka kwa afisa mmoja mwandamizi katika timu hiyo. Meneja wa klabu ya Houston Rockets,  Daryl Morey,  alituma ujumbe kupitia mtandao wa  Twitter akiunga mkono waandamanaji wanaounga mkono demokrasia huko Hong Kong. Kutokana na hatua hiyo kampuni za China zilisitisha ufadhili wao na ule wa runinga kwa timu hiyo.

Leave a Comment