×

Vijana Msiogope Kugombea 2020; Uongozi Si Wa Matajiri Tena

 

MTU yeyote aliyenipatia pesa kushinda urais anyooshe mkono!” Hiyo ilikuwa ni kauli ya Rais Dk. John Pombe Magufuli Ikulu mara baada ya kushinda urais wakati akiongea na wafanyakazi aliowaalika Ikulu.

 

Kauli hii ilinifurahisha sana mimi binafsi lakini pia najua na Watanzania wengine wengi walioisikia pia walifurahi sana. Nilifurahi kwa sababu ilikuwa imefungua mlango wa Watanzania kuanza kupata viongozi sahihi wa kuliongoza taifa letu, hasa vijana wengi ambao waliwekwa pembeni na siasa za nchi hii kwa sababu ya umaskini wao, na uongozi wa nchi hii kubaki mikononi mwa watu wenye nacho.

 

Nilishawahi kushiriki mbio za ubunge mwaka 2010. Naweza kukiri kabisa kwamba siasa ni fedha na uchaguzi ni matumizi, ilikuwa si rahisi hata kidogo kwa mtu asiye na fedha kuumudu mchakato wa kushinda ubunge!

 

Siwezi kukataa, siasa ni fedha, popote duniani, ndiyo maana huko Marekani akina Obama walilazimika kufunga machangizo ili kuweza kugharamia kampeni zao. Ninachokataa hapa ni watu kununua uongozi katika taifa, watu kununua wapiga kura. Nakataa kabisa chaguzi kugubikwa na rushwa.

 

Kwa muda mrefu kitendo hiki kilifanya uongozi wa taifa letu kuingia mikononi mwa matajiri, vijana wadogo kutoka katika vyuo vikuu vyetu, wafanyakazi wa kada za chini kama walimu, lakini wenye uwezo mkubwa wa kuongoza na pengine uadilifu wa kutosha waliwekwa pembeni kwa sababu tu ya umaskini wao.

 

Rais Magufuli kutamka tu maneno hayo mbele ya macho ya Watanzania wote ilifungua milango kwa watu wasio matajiri kama ilivyokuwa kwake sasa kushiriki katika uongozi wa taifa letu.

 

Mwaka 2020, kuna uchaguzi mkuu wa rais na wabunge; naandika makala haya leo kuwasisitiza vijana katika nchi hii kujitokeza kugombea nafasi yoyote ile, wasijidharau kwa sababu hawana utajiri. Nchi yetu inahitaji viongozi wenye upeo na uwezo, sio matajiri, na Rais Magufuli ametuonesha njia; ni ruhusa kugombea, ni haki ya kila mmoja wetu na rushwa itadhibitiwa.

 

Uchaguzi wa ubunge safari hii ni wa wajumbe; ambao wengi huchukulia kipindi cha uchaguzi kama msimu wa mavuno kutoka kwa wagombea, ambao baadhi tayari wameandaa mikono yao kupokea takrima ili wapitishe majina ya wagombea waliowapatia fedha bila kujali ni viongozi wa kweli ama la, hii ni mbaya na inawanyima nafasi baadhi ya wagombea wasio na uwezo wa kutoa chochote.

 

Jambo moja muhimu ambalo wajumbe hawa wanapaswa kulikumbuka ni kwamba wamepewa dhamana hii na wananchi walio wengi ili wawapitishie majina ya viongozi watakosaidia kuondoa kero na matatizo yao na wanaofahamu wanaowataka.

 

Kitendo cha wajumbe kuwapelekea wapiga kura mtu wasiyemtaka kwa sababu tu aligawa fedha kwa wajumbe, kinaudhi na hakika kitasababisha hasira na madhara makubwa hata ya kupoteza majimbo, hapa wajumbe wanapaswa kutumia hekima na busara.

 

Hivyo basi, kama Mtanzania anayeipenda nchi yake na kuamini sote tuna haki sawa, naandika makala haya leo kuwaomba wajumbe nchini kote waheshimu matakwa ya walio wengi kipindi cha kupiga kura kuchagua wagombea kitakapowadia, wananchi wote pia wakiwemo vijana wa nchi hii nawaasa wasiwe na hofu ya kuingia katika kinyang’anyiro hiki eti kwa sababu tu hawana utajiri wa kushawishi wapiga kura.

 

Rais wetu mpendwa amekwishaonesha mfano kwamba unaweza kuwa kiongozi katika nchi hii bila kurubuni watu kwa fedha na hii ndiyo njia sahihi ya kujipatia viongozi bora watakaolipeleka taifa hili mbele.

 

Enzi zile za awamu ya tatu ya Rais Benjamin William Mkapa, jambo hili lilisimamiwa vyema, nakumbuka kuna majina ya baadhi ya wagombea tena wenye ukwasi mkubwa yalikatwa kwa sababu tu walitumia fedha nyingi kushawishi wapiga kura, kama Rais Mstaafu Mkapa alifanya hivyo basi huyu tuliyenaye anaweza kulifanya jambo hilo mara mbili zaidi yake; vijana jitokezeni bila kusita, sote tunao uwezo wa kuwa viongozi hata kama tunatokea familia maskini.

 

Matarajio yangu mwaka 2020 itakapofika vijana wengi nchi nzima watajitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na hatimaye kushika madaraka katika nchi hii ili wapate kuitumikia nchi yao.

 

Rais wetu mpendwa anaonesha imani kubwa sana na vijana, walioko madarakani leo kina Paul Makonda, Mheshimiwa Suleiman Jafo, Ali Hapi, Mrisho Gambo, Joketi Mwegelo na wengineo wengi ambao siwezi kuwataja hapa kwa majina wamemthibitishia rais wetu kwamba vijana wanaweza.

 

Na hii si kwa Tanzania pekee, duniani kote vijana wadogo wamekuwa chachu ya mafanikio makubwa katika uongozi. Nchini Finland, hivi karibuni tu rekodi ya dunia imewekwa. Mwanadada Sanna Mirella Marin amechaguliwa waziri mkuu wa nchi hiyo, Desemba 10, 2019 akiwa na umri wa miaka 34 tu! Ameweka rekodi ya kuwa kiongozi wa ngazi hiyo mdogo zaidi duniani na kinachoshangaza zaidi ni kwamba ni mwanamke!

 

Kijana mdogo wa kike ameweza kuwa waziri mkuu wa taifa lenye nguvu kama Finland! Kwa nini kijana wa Kitanzania uone kwamba haiwezekani? Natoa wito kwa vijana kote nchini, changamkieni fursa hii, jitokezeni kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwa sababu jamii inawategemea na inawaamini.

 

Mwisho nampongeza sana Rais John Pombe Magufuli kwa uamuzi huu wa kupunguza matumizi ya utajiri kwenye chaguzi, hakika amewakumbuka watoto wa maskini kama yeye ili nao wapate haki ya kuongoza taifa. Najua atapata viongozi wa kweli wenye uchungu na nchi hii watakaomsaidia katika safari kuelekea kwenye ndoto ya Tanzania mpya.

 

Asanteni kwa kunisoma na Mungu awabariki sana!

DIARY Ya Shigongo

Leave a Comment