
ASASI isiyo ya kiserikali ya Human Dignity and Environmental Care Foundation (HUDEFO) inayojihusisha na utu na mazingira jana iliandaa mdahalo uliohusu utunzaji wa mazingira yakiwemo matumizi ya nishati jadidifu.

Mdahalo huo ulizihusisha taasisi za kiserikali, likiwemo shirika la ugavi wa umeme nchini (Tanesco), wakufunzi na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na vyuo vingine. Pia kulikuwa na taasisi zingine za dini, benki na nyinginezo.

Mdahalo huo pia ulihudhuriwa na viongozi wa serikali za mitaa ambao ni wadau wakubwa wa mazingira katika jamii.

Katika mjadala huo mambo mbalimbali yalijadiliwa kuhusiana na matumizi bora ya nishati jadidifu na madhara ya kutumia nishati zinazosababisha uharibifu wa mazingira.

Imeelezwa katika kongamano hilo kuwa baadhi ya nishati zinazosababisha uharibifu wa mazingira ni pamoja na kuni na mkaa.

Ilifahamika pia kuwa kwa mwaka watu zaidi ya 22,000 ulimwenguni wanapoteza maisha kwa kuvuta moshi kutokanana kutumia kuni.

Akizungumza kwenye mdahalo huo muanzilishi wa HUDEFO, Sara Pima, amesema tatizo kubwa na uharibifu wa mazingira lipo vijijini ambapo wananchi wengi hawana elimu ya kutosha ya mazingira.

Pima amesema katika kuokoa mazingira, HUDEFO itakuwa ikifanya midahalo hiyo kila mwezi ambapo watakuwa wakizunguka sehemu mbalimbali.


Mmoja wa washiriki wa mdahalo huo akitoa mchango wake.
HABARI/PICHA: RICHARD BUKOS /GPL