
NGUZO pekee kwenye kikosi cha Real Madrid kwa sasa ni safu yake imara ya ulinzi ambayo imekuwa ikifanya kazi kubwa kuliko hata nyingine zote za ligi hiyo.
Madrid kwa msimu huu imeonekana kuwa na kasi ya hali ya juu sana ya kuwania ubingwa wa ligi hiyo kubwa zaidi Ulaya ikiwa nafasi ya pili kwenye ligi na pointi 37.
Wakati Madrid wanafikiri kuhusu ubingwa walifanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha wanakuwa na safu imara ya ulinzi.
Ndiyo maana pamoja na timu hiyo kuwa na kipa Keylor Navas, pia ilipambana na kumpata Thibaut Courtois ambaye kwa sasa anaonekana kuwa mahiri zaidi.
Mashabiki wengi hawakuelewa kwa nini Madrid walifanya hivyo, lakini sasa sura na sababu ya kufanya hivyo imeshaonekana.
Hata hivyo, kwa kipindi cha miezi 16 kwenye La Liga, Courtois na safu yake ya ulinzi wameonekana kuwa imara sana, siyo kwenye La Liga tu, hata kwenye michuano mingine mikubwa Ulaya ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kipa huyo amekuwa ndiye kiongozi sahihi kwenye timu hiyo na anaonekana anaweza kuwa mhimili mkubwa kwenye ubingwa wa ligi na Uefa msimu huu.
Ukiwa ni nusu ya msimu kwa sasa vijana hao wa kocha Zinedine Zidane, wameonekana kuwa timu ya pili kwa safu bora ya ulinzi kwenye La Liga.
Wakiwa wameruhusu mabao 12 tu kwenye michezo 18, ambayo wamecheza wakiwa wanalingana na Athletic Bilbao.
Nafasi ya kwanza kwenye Ligi hiyo inashikwa na Atletico Madrid ambao wameruhusu mabao 11 tu msimu huu.
Celta Vigo, Valladolid, Villarreal, Levante, Granada, RCD Mallorca, Real Sociedad, Alaves, Espanyol na Valencia ndiyo timu pekee ambazo zimefanikiwa kumfunga Courtois msimu huu, huku Barcelona wakiwa walimaliza mechi yao bila kutikisa nyavu za Madrid.
Lakini inaonekana kuwa sifa pekee siyo kwa kipa tu, bali hata safu nzima ya ulinzi ambayo imekuwa ikiongozwa na Sergio Ramos, ambaye amekuwa mhimili mkubwa wa Madrid kwa miaka mingi.
Katika wachezaji 26 wa Madrid, 10 wamekuwa wakicheza kama walinzi akiwemo Casemiro ambaye anakuwa wa 11.
Hii imekuwa ikiwafanya Madrid kutokuwa na upungufu wa mara kwa mara kwenye safu yao ya ulinzi na ndiyo kitu pekee ambacho kimekuwa kikiifanya timu hii kuonekana kuwa imara hata inapokutana na timu kubwa na zinazoshambulia kwa muda mrefu.
Timu hiyo imekuwa ikiruhusu wastani wa mashuti 8.4, lakini wachezaji wake wamekuwa wakipiga takolini 15.5 na kupokonya mipira mara 10 kwenye kila mchezo.
Kwa mchezaji mmojammoja, Sergio Ramos amekuwa akionekana kuwa imara sana kwa kipindi kirefu ambacho amekuwa kwenye timu hiyo.
Ramos amefanikiwa kucheza dakika zote kwenye La Liga msimu huu akiwa ametumika kwenye dakika 1,590, akiwa na wastani wa takolini 1.4 kwa kila mchezo.
Lakini amekuwa akikutana na watu wengine muhimu sana kwenye timu hiyo akiwemo Casemiro, Dani Carvajal na Raphael Varane.
Casemiro amekuwa na wastani wa takolini 3.8, kwenye kila mchezo, akiwa ndiye kinara kwenye timu hiyo.
Hawa wamekuwa wakionekana kuwa mhimili muhimu sana kwenye timu hiyo wakiwa wanasaidiwa na wachezaji wengine vijana ambao wamekuwa wakiingia kwenye timu na kutoka.
Wachezaji makinda kama Eder Militao, Alvaro Odriozola na Ferland Mendy nao wamekuwa wakiifanya timu hii ionekane kuwa imara kwa kuwa kila wanapopata nafasi wamekuwa wakifanya mambo makubwa uwanjani.
MADRID, Hispania