
KATIKA hali isiyo ya kawaida, mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Kambiala Kata ya Msanzi wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani humo kwa tuhuma za kumkata sehemu za siri za mwanaye wa kiume mwenye umri wa siku nane na kumsababishia jeraha.
Vilevile, katika tukio jingine, kijana anayedaiwa kumuua mama yake kwa mpini wa jembe kufuatia mgogoro wa ardhi naye amekamatwa.
Akiongea na waandishi wa habari katika viwanja vya polisi mkoa wa Rukwa, Kamanda wa polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Justine Masejo, amesema dada wa mama mzazi wa mtoto huyo alibaini kufanyiwa ukatili mtoto alipofika nyumbani kumpelekea mdogo wake chakula na kukuta mtoto akilia akiwa peke yake wakati huo mama yake akiwa ametoka. Mama wa mtoto huyo aliporejea na kuulizwa kuhusu kukatwa mwanaye sehemu za siri alikana kuhusika.
Pia, kijana mmoja anashikiliwa na polisi mkoani Rukwa baada ya kudaiwa kumpiga kwa mpini wa jembe kisogoni mama yake mzazi na kusababisha kifo kutokana na mgogoro wa ardhi wa ekari 16 za familia katika kijiji cha Kilembo kata ya Kalambanzite wilaya ya Sumbawanga.