
MWANDISHI wa habari nchini, Erick Kabendera, amewashukuru Watanzania kwa kuuungana na familia yake kuomboleza kifo cha mama yake mzazi Verdiana Mjwahuzi (80).
Verdiana alifariki dunia Jumanne iliyopita, Desemba 31, 2019, katika Hospitali ya Rufaa ya Amana jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa siku mbili kwa matibabu.
Leo Ijumaa Januari 2, 2020, kulifanyika Ibada ya kuuaga mwili wa Verdiana katika Kanisa Katoliki la Mt. Francis Xavier Chang’ombe, Temeke, Dar es Salaam, ambapo mamia ya waombolezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania wamejitokeza.

Jana Alhamisi, maombi ya Kabendera ya kuhudhuria ibada hiyo ya kuaga mwili wa mama yake yaligonga mwamba baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuyatupilia mbali ikisema haina mamlaka hayo na hayawezi kukatiwa rufaa.
Baada ya uamuzi huo, Kabendera alirejeshwe gereza la Segerea anakokaa tangu Agosti 5, 2019, kutokana na mashtaka matatu anayokabiliwa nayo likiwamo la uhujumu uchumi na utakatishaji fedha zaidi ya Sh 173 milioni.
Hata hivyo, Kabendera alituma salamu katika ibada hiyo ambazo zilisomwa kanisani hapo na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, ambazo alipewa na Jebra Kambole, mwanasheria wa Kabendera.
Katika salamu Zitto alisema (kwa niaba ya Kabendera):

Yeye, kama ambavyo mtoto yeyote angetaka, alitamani kuwa nanyi hapa katika wakati huu lakini kwa sababu ambazo nyote mnazifahamu, ameshindwa kuungana nasi hapa.
Siku hizi tatu zimekuwa ngumu sana kwa Erick. Katika jambo gumu ambalo nimewahi kulifanya kama mwanasheria ni hili la kumpelekea Erick taarifa za kufiwa na mama yake.
Anapitia katika wakati mgumu sana na nawaomba mumweke katika maombi yenu ili hatimaye kikombe hiki anachokinywa kwa sasa kimwepuke.
Erick amejaribu kuandika ujumbe kwenu ambao alitaka niusome mbele yenu. Amepata taabu sana kuandika na kufuta ili kufikisha ujumbe anaoutaka. Ameniambia ametumia karibu kurasa 20 kuandika ujumbe huu usiku mzima wa jana. Anaandika na kufuta.
Ndiyo sasa nimejua kwamba kumbe kuna wakati hata waandishi mahiri nao hukwama kuandika!!!!
Hatimaye ameweza kuandika kwa ufupi yafuatayo.

Naomba niwasomee, alisema Zitto.
“Kuna mama mmoja.
Anafariki mara moja,
msiba mara moja.
Uchungu wa kuondokewa na mama ni mkubwa sana, hasa anapokuwa ameondoka na umeshindwa kumuaga kama ilivyotokea kwangu.
Hata hivyo nimefarijika kwa Watanzania wote walioguswa na msiba huu bila kujali itikadi zao za kisiasa na kidini na kunisaidia kumsitiri mama yangu.
Upendo huu umeonyesha nchi ambayo nimeipenda na naipenda kutoka moyoni. Shukrani za dhati ziwafikie watu wote kwa upendo wao na ushiriki wao kufanikisha msiba wa mama yangu.
Mwenyezi Mungu na awabariki sana na kuwaongezea pale mlipopunguza kwa ajili yangu.
Mtuombee.
Uchungu wa kuondokewa na mama ni mkubwa sana, hasa anapokuwa ameondoka na umeshindwa kumuaga kama ilivyotokea kwangu.
Hata hivyo, nimefarijika kwa Watanzania wote walioguswa na msiba huu bila kujali itikadi zao za kisiasa na kidini na kunisaidia kumsitiri mama yangu.
Shukrani za dhati ziwafikie watu wote kwa upendo wao na ushiriki wao kufanikisha msiba wa mama yangu. Mwenyezi Mungu na awabariki sana na kuwaongezea pale mlipopunguza kwa ajili yangu. Mtuombee.”