
KILA upande unauambia upande mwingine, wanakaa. Ndiyo, hii ni ‘bato’ ya mashabiki wa Simba na Yanga ambao leo Jumamosi timu zao zitapambana kusaka heshima na pointi tatu muhimu.
Mechi hii ya kukata na shoka itaanza saa 11:00 Jioni pale Uwanja wa Taifa na itachezeshwa na mwamuzi mwanamke, Jonesia Rukyaa kutoka mkoani Kagera ambaye anatajwa na wengi kwamba amekuwa mkali na mwepesi kutoa kadi, atasaidiwa na Sudi Lila na Hamis Chang’walu (wote kutoka Dar).

Elly Sasii ambaye naye anatoka Dar, atakuwa mwamuzi wa akiba wa mchezo huo, huku kamishna akiwa Khalid Bitebo kutoka Mwanza na mtathmini wa waamuzi ni Sudi Abdi wa Arusha.
TFF imemtangaza mwamuzi huyo mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwamba ndiye ataamua mchezo huo ambao awali kulikuwa na mpango wa kuwepo kwa VAR, lakini sasa mpango huo haupo.
Mpaka jana mashabiki kibao wa Simba na Yanga walikuwa wakitambiana mitaani kila mmoja akisema ni lazima ammalize mpinzani wake lakini sasa leo hadi kufikia saa 12 jioni na dakika kadhaa hivi kila upande utajua nani mbabe.

Makocha wa timu zote, Sven Vanderbroeck wa Simba na Charles Boniface Mkwasa wa Yanga wametambiana kupeleka vilio leo. Wakizungumza mbele ya Waandishi wa Habari, Sven alisema kuwa kwa upande wake anatarajia kuona mchezo mzuri kutokana na ubora wa timu yake lakini anawaheshimu wapinzani wake, Yanga.
“Ni mechi kubwa na ina presha pia, naamini itakuwa mechi nzuri na ngumu. Tunaiheshimu Yanga lakini tumejipanga kuhakikisha tunaondoka na pointi zote tatu kwa sababu hilo ndiyo lengo letu kubwa katika mchezo wa kesho (leo).

“Lakini nje ya hapo wachezaji wapo vizuri isipokuwa ni kwa Miraji (Athumani) na Rashid (Juma) hawatakuwa sehemu ya mchezo kwa kuwa ni majeruhi lakini wengine wote wako vizuri na jana (juzi) walifanya mazoezi jioni, tunachosubiria ni kuona tunapataje ushindi siku ya mchezo,” alisema Vanderbroeck.
Kwa upande wake Mkwasa alisema, mechi ya leo itakuwa ya kawaida kama zilivyo mechi nyingine lakini kinachotofautisha ni ukongwe wa timu zenyewe na kwamba wao wametoka kucheza mechi ngumu hivyo wako vyema. “Inasemwa kwamba Simba imeshinda mechi nne mfululizo na sisi tumejiandaa kuwafunga ili wasiendelee kushinda mechi mfululizo.

“Tunaamini mechi itakuwa ngumu lakini kwa kuwa tunaiheshimu Simba kama tunavyoziheshimu timu nyingine, nimecheza na nimekaa kwenye benchi kama mwalimu katika mechi nyingi dhidi ya Simba, hivyo ninaamini tutashinda,” alisema Mkwasa.
Katika mchezo huo, Yanga watawakosa Lamine Moro ambaye ana kadi tatu za njano na mshambuliaji, Tariq Seif ana asimilia 50 za kucheza kutokana na kusumbuliwa na nyama za paja.
Vikosi ambavyo vinatarajiwa kupangwa leo ni; Kwa upande wa Simba wanaotarajiwa kuanza ni; kipa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Hussein Mohammed ‘Tshabalala’, Pascal Serge Wawa, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Deo Kanda, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Clatous Chama na Francis Kahata. Yanga; Farouk Shikalo, Mustafa Selemani, Ally Mtoni ‘Sonso’, Andrew Vicent ‘Dante’, Kelvin Yondani, Abdulaziz Makame, Mapinduzi Balama, Papy Tshishimbi, Yikpe Gnamien, Ditram Nchimbi na Patrick Sibomana. Kunaweza kuwa na mabadiliko kutokana na maendeleo ya wachezaji wa timu zote ambao jana walifanya mazoezi ya mwisho kabla ya leo kutinga Taifa.