×

Simba Vs Yanga… Mtu na Mtu

 

MAJIGAMBO, mikwara na kejeli za watani wa jadi Simba na Yanga zinamalizika leo wakati timu hizo kongwe zitakapokuwa uwanjani zikipambana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.

 

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa kutokana na kila timu kufanya maandalizi ya kutosha ili kuhakikisha wanapata ushindi.

 

Katika pambano hilo, vikosi vya timu zote vimebadilika tofauti na msimu uliopita baada ya kuviimarisha kwa kufanya usajili kwenye dirisha kubwa la usajili kabla ya Desemba 16, mwaka jana dirisha dogo la usajili kufunguliwa na Yanga kuonekana kufanya usajili wa haraka wa wachezaji watano.

 

Wachezaji ambao Yanga tayari uhakika wamesaini mkataba wa kuichezea timu hiyo ni Ditram Nchimbi, Adeyum Salehe, Yikpe Gnaimen, Tariq Seif na Haruna Niyonzima aliyetua juzi na kujiunga na kambi ya timu hiyo moja kwa moja kujiandaa na mchezo huo wa watani.

Wakati pambano hilo likisubiriwa kwa hamu kubwa, vita na uhondo wa pambano utakuwepo kwa wachezaji hawa watakapokutana uwanjani wakipambana uwanjani.

 

YONDANI VS KAGERE

Kelvin Yondani na Meddie Kagere wamekutana mara mbili katika ‘derby’ ya Kariakoo kwenye msimu uliopita wa ligi ambao Kagere alifanikiwa kufunga bao katika ushindi wa bao 1-0 walioupata.

 

Walipokutana msimu uliopita, vita kubwa ilikuwepo kwa Yondani kupambana kumzuia na kumpunguza makali Kagere huku yeye akipambana kupenya kwenye safu ya ulinzi ya Yanga, hivyo leo watakapokutana vita kubwa itakuwepo katika pambano hilo.

 

WAWA VS TARIQ

Hapa itakuwepo kazi kwelikweli, kwani wote wawili Tariq Seif na Pascal Wawa wote ni wachezaji wanaotumia nguvu na akili nyingi ndani ya uwanja katika kupambana.

 

Ni mara yao ya kwanza wanakutana katika mchezo huo ambao kwa Tariq hana uzoefu na derby hii kwani ni mchezo wake wa kwanza kucheza tangu ajiunge na timu hiyo katika dirisha hili dogo. Itakuwa mechi ya pili kama atacheza kwani ya kwanza ilikuwa dhidi ya Biashara na akafunga bao moja.

 

KAPOMBE VS SIBOMANA

Patrick Sibomana huu ni mchezo wake wa kwanza kucheza ‘derby’ ya Kariakoo tangu ajiunge na Yanga msimu huu lakini kwa Shomari Kapombe tayari ameshazoea kutokana na kuwahi kucheza mara kadhaa akiwa na timu yake.

 

Katika mchezo huo, Kapombe anahitaji kucheza kwa tahadhari ya kutompa nafasi ya kupiga krosi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupiga mipira hiyo kwa washambuliaji wake, lakini pia Sibomana naye anatakiwa kucheza kwa tahadhari ya kushambulia na kulinda goli lake kutokana na uwezo mkubwa alionao Kapombe katika kuanzisha mashambulizi kwenye lango la timu pinzani.

 

NYONI VS YIKPE

Gnamien Yikpe ni kati washambuliaji wanaotajwa na Yanga katika kuelekea pambano hilo ambaye amebeba matumaini makubwa kwa mashabiki wa timu hiyo, lakini atakutana na beki mkongwe anayecheza kwa kutumia akili nyingi ambaye ni Erasto Nyoni.

 

Katika mchezo huo, Nyoni anatakiwa kucheza kwa uangalizi mkubwa katika dakika za mwanzo kwa kumsoma mshambuliaji huyo mwenye mwili mkubwa. Yikpe naye anatakiwa kuwa makini kwani anakwenda kukutana na kati ya mabeki bora wa Simba. Hivyo tunatarajia kuona vita kubwa katika mchezo huu.

 

MAKAME VS MZAMIRU

Vita kubwa hapa kwenye safu ya kiungo itakayomkutanisha Abdulaziz Makame wa Yanga na Mzamiru Yassin ambaye ni kiungo bora hivi sasa kwenye kikosi cha Simba.

Katika mchezo huo ushindi wa kila timu upo hapa kwenye safu ya kiungo ambao ni wapishi wa washambuliaji katika pambano hilo na yule atakayetimiza majukumu yake vizuri ya kupiga pasi za mabao, basi ndiye atakuwa shujaa lakini hapa kutakuwa na kazi kubwa kwelikweli.

 

MKUDE VS TSHISHIMBI

Siyo mara yao ya kwanza wanakutana katika Derby ya Kariakoo, wameshakutana kwenye misimu miwili iliyopita ya ligi na wote wanajuana aina yao ya uchezaji, hivyo hapa napo kutakuwepo na kibarua kigumu.

Kati ya wachezaji hao, yeyote anaweza kung’ara kwa kuonyesha kiwango kizuri au kutengeneza nafasi za mabao.

 

SHEVA VS ABDUL

Beki wa Yanga, Juma Abdul ana kibarua kigumu mbele ya kiungo mshambuliaji wa Simba Miraji Athumani ‘Sheva’ kutokana na kasi aliyonayo pindi anapokuwa anakokota mpira, ni mchezaji hatari pale anapokuwa na mpira na wala hana woga kwa mabeki.

Ana mabao sita aliyofunga msimu huu ndani ya ligi pia ametengeneza nafasi moja ya bao kati ya yale 27 ambayo Simba imefunga.

 

Wakati Sheva akiwa na sifa hizo, Abdul yeye anajivunia uzoefu alionao wa kucheza derby hizo ambaye ni hatari kwa mipira ya faulo, kona na krosi kwa washambuliaji wake anahitaji uangalizi wa hali ya juu, hivyo Sheva ndani ya wakati mmoja anatakiwa afanye majukumu mawili ya kusaidia kukaba ili Abdul asipate nafasi ya kushambulia na kuanzisha mashambulizi.

 

NIYONZIMA VS TSHABALALA

Haruna Niyonzima kama hataanza katika kikosi cha kwanza basi ataanzia benchi na kucheza namba saba kama kiungo anayetokea pembeni akipambana na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye ni nahodha msaidizi wa Simba.

 

Wachezaji wote wanajuana waliwahi kucheza pamoja Simba msimu uliopita, upo uwezekano mkubwa wa Niyonzima kucheza kwa lengo la kuwavuruga wapinzani wao kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuchezesha timu.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

 

Leave a Comment