×

Jokate, K-Lynn Wang’ara Afrika

DAR: Tanzania imeingia kwenye historia ya kipekee baada ya warembo wawili, Jacqueline Mengi Ntuyabaliwe ‘K-Lynn’ na Jokate Urban Mwegelo kung’ara na kuwekwa kwenye orodha ya Wanawake 30 Bora katika kipindi cha miaka 10 barani Afrika, Gazeti la IJUMAA limeinyaka.  Wawili hao wametajwa na mtandao wa masuala ya mitindo na urembo wa nchini Nigeria unaoitwa Stylerave ambapo mjasiriamali Mtanzania, K-Lynn ameongoza kwenye orodha hiyo.

Jokate ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, katika orodha hiyo amewekwa nafasi ya 16. K-Lyyn ambaye ni Miss Tanzania mwaka 2000, katika tovuti hiyo ametajwa kutokana na kujishughulisha kwake na biashara ya samani za majumbani kupitia Kampuni ya Amorette Ltd yenye makao yake makuu nchini Tanzania.

Kwa sasa kampuni hiyo inafanya vizuri Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla. Pia K-Lynn ametajwa kutokana na kutoa misaada kwa watoto wadogo wa shule za msingi kupitia taasisi yake ya Dk Ntuyabaliwe Foundation ambayo imekuwa na mchango mkubwa wa kujenga maktaba za watoto pamoja na vifaa mbalimbali vya shule na kukarabati miundombinu ya shule.

Aidha, Jokate ametajwa katika orodha hiyo kutokana na harakati ya kumkomboa mtoto wa kike kupitia elimu, kutokana na kuanzisha kampeni mbalimbali za kutokomeza ziro, kupinga ukatili wa kijinsia na kuanzisha miradi ya kuwakwamua vijana katika tatizo la uhaba wa ajira.

Hata hivyo, wakizungumza hatua hiyo, pamoja na kuelezea furaha yao kuhusu orodha hiyo, pia wametoa wito kwa wasichana warembo kutumia urembo wao kubadilika na kufanya mambo yanayoweza kusaidia maendeleo yao na ya jamii. 

JOKATE ANAFUNGUKA

“Harakati zangu za kujitoa kwenye jamii kuhamasisha vijana kwenye masuala ya maendeleo na kubuni vitu mbalimbali vyenye tija vinaacha alama chanya,” alisema Jokate katika mahojiano na Gazeti la Ijumaa kuhusu ishu hiyo.

Aidha, alisema siri kubwa kwake ni kujiendeleza kielimu. “Kikubwa pia nilifanya uamuzi wa kujiendeleza elimu ya juu zaidi na hivyo kunipa nafasi ya kuwa kiongozi na pia kufanya vizuri kwenye masomo na kushika nafasi mbalimbali za uongozi tangu shule na kwenye jamii,” alisema Jokate.

K-LYYN

Kwa upande wake, K-Lyyn aliliambia Gazeti la IJUMAA kuwa, furaha yake siyo kwa kutajwa kuwa mwanamke mrembo na bora Afrika, bali pia ni kutajwa katika warembo wenye mafanikio kwenye shughuli wanazozifanya, wanaojali kuhusu jamii zao na mazingira yanayowazunguka.

“Wametaja sababu ya kuwa namba moja kuwa ni kutokana na kazi zangu ubunifu wa samani na tuzo nilizopata kupitia kazi zangu, pia wamezungumzia sana kuhusu kazi ninazozifanya kupitia Taasisi ya Dk Ntuyabaliwe, ambayo nilianzisha kwa ajili ya kukarabati maktaba na kutoa vitabu kwa shule za msingi Tanzania.

“Inaleta faraja sana kuona kwamba kazi tunazozifanya hapa Tanzania, lakini zinavuka nje ya mipaka ya nchi yetu, inaendelea kunipa moyo kusaidia jamii inayonizunguka na nimechagua kufanya kazi kwa ajili ya watoto hasa ukizingatia mimi ni mama wa watoto wa miaka saba,” alisema K-Lynn.

Aidha, alitoa wito kwa wanawake na wasichana kujitambua na kutumia nafasi yao katika jamii, kujua wanataka kufanya nini na kusimamia katika kile wanachokiamini.“Kila mtu ana nafasi yake na anaweza kufanya kitu ambacho kinaweza kuwa na manufaa na kuleta furaha.

“Pongezi kwa wanawake wenzangu ambao wamewekwa kwenye orodha hiyo, natumaini hii itakuwa chachu kwa wanawake wenzangu na wasichana wanaokua na kujitambua kwamba urembo siyo wa sura tu, bali pia unatakiwa utoke ndani uwe na nafasi ya kufanya vitu vinavyoonekana na kuleta maendeleo kwako na ndani ya jamii inayokuzunguka,” alisema K-Lynn.

Stori: IMELDA MTEMA, Ijumaa

Leave a Comment