Meya wa Ubungo, Boniface Jacob ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wimbo unaotumiwa katika shughuli na mikutano ya CCM wenye maneno ‘wapinzani tuwalete tuwachane tuwatupe’, unawahamasisha wananchi kuwanyima kura wapinzani.
Jacob ambaye pia ni diwani wa Ubungo ametoa kauli hiyo leo Jumatano Januari 22, 2020 wakati akitoa ushahidi katika kesi hiyo ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema mbele ya hakimu mkazi mkuu, Thomas Simba.
Meya huyo ambaye ni shahidi wa 10 katika kesi hiyo alieleza hayo baada ya kuulizwa na wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala anaelewa nini kuhusu maneno yanayotumiwa wakati wa uchaguzi ya kuchinja na kichinjio (kitambulisho cha mpigakura).
Viongozi hao wa Chadema wanakabiliwa na mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi wanayodaiwa kuyatenda Februari 16, 2018 katika viwanja vya Buibui, Mwananyamala katika mkutano wa kufunga kampeni za ubunge wa Kinondoni.
“Kuna kawimbo umekasikia kana maneno wapinzani tuwachukue tuwachane tuwatupe, kwa uelewa wako maneno hayo yana maana gani,” amehoji Kibatala.
Akiongozwa na Kibatala, meya huyo amesema kichinjio kama ilivyoainishwa kwenye mashtaka ni kitambulisho cha kupiga kura kinachotumika katika chaguzi mbalimbali na kwamba kuchinja ni kunyima kura.
“Harambee, harambee, harambee, wapinzani tuwalete, tuwachane tuwatupe, CCM tuwalete tuwakumbatie tuwabusu,” amesema Jacob akirejea kutaja maneno yaliyo katika wimbo huo ulioimbwa na Kapteni John Komba (marehemu).
Awali, wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi alipinga swali kuhusu wimbo huo lakini Hakimu aliruhusu swali kuulizwa na shahidi huyo akaeleza kuwa wimbo huo unalenga kuwanyima kura wapinzani.