
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni katika mkutano wake maalum wa baraza leo Alhamisi Januari 23 mwaka 2020 limejadili na kuhidhinisha kwa kauli moja bajeti yake. Bajeti hiyo ni Tshs 170,918,524,100/= kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ambapo Tshs 127,967,212,100/= ni mapato ya ruzuku kutoka Serikali Kuu zikijumuisha Tshs 57,018,968,680/= kwa ajili ya mishahara , Tshs 1,689,501,000/= za matumizi mengineyo na Tshs 69,258,742,520/= za miradi ya maendeleo.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mheshimiwa Benjamini Sitta amebainisha kuwa ili kuboresha maisha ya wakazi wa Kinondoni imeandaa mpango wa mwaka 2020/2021 na mpango wa muda wa kati 2020/2021 – 2022/2023 unaolenga kukuza uchumi na kupunguza umaskini na kufikia maendeleo endelevu ya kijamii, kiuchumi na mazingira kwa wananchi wake.

Mstahiki Meya Sitta amesema baadhi ya miradi iliyotengewa fedha kwa mapato ya ndani ya Manispaa katika mwaka wa fedha 2020/2021 ni pamoja na ukamilishaji wa kituo cha kisasa cha daladala Mwenge kwa milioni 500, ukamilishaji wa ujenzi wa uwanja wa mpira wa Mwenge kwa shilingi milioni 500, ujenzi wa kituo cha daladala na Soko la Tegeta Nyuki kwa bilioni 3.5, ujenzi wa kituo kisasa cha Bunju B, kwa milioni 600, ujenzi wa maabara, famasia, rediolojia na ununuzi wa gari la kubeba wagonjwa katika Hospitali ya Mabwepande kwa bilioni 1 na ujenzi wa incinerator kubwa kwa ajili ya kuchoma taka za vituo vyote vya kutolea huduma za afya kwa bilioni 1.5.

Meya Sitta (katikati) akiwa na Naibu wa George Manyama (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Kinondoni, Dkt. Patricia Henjewele.
HABARI:NEEMA ADRIAN ,PICHA: RICHARD BUKOS