
ROMELU Lukaku amekuwa katika kiwango bora sana tangu alipotua Inter Milan lakini pamoja na uwezo wa kufunga mabao anaoendelea kuuonyesha, amefunguka kuwa kocha wake, Antonio Conte, amewahi kumkosoa na kumwambia yeye ni takataka tu mbele ya kikosi kizima.
Matusi hayo ya Conte yalitoka baada ya sare ya nyumbani dhidi ya Slavia Prague kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, matokeo ambayo yalisababisha Inter ishindwe kusonga hatua ya mtoano.
“Nilicheza vibaya sana, na (Conte) aliniambia nilikuwa takataka. Aliniambia maneno hayo mbele ya kikosi kizima,” alisema Lukaku.
“Kama upo sahihi au umekosea, ana kawaida ya kukuambia moja kwa moja akikuangalia usoni, alisema kama nikirudia kucheza hovyo namna ile anaweza kunitoa hata baada ya dakika tano uwanjani.
“Alinipotezea hali ya kujiamini, lakini wakati huohuo aliniamsha, hufanya hivyo kwa kila mmoja, bila kujali wewe ni nani, kwake kila mtu ni sawa.”
Lukaku hadi sasa ameifungia Inter Milan mabao 18 katika michezo 26 ya michuano yote, akiwa mmoja wa mastaa wa kikosi hicho wanaofanya vizuri.
MILAN, Italia