
IMEELEZWA kuwa kichapo cha mabao 2-1 walichopokea Mwadui FC kutoka kwa Simba kimepeperusha milioni mbili zilizokuwa mezani kwa ajili ya hamasa kwa wachezaji wa Mwadui FC.
Mwadui ilishindwa kufurukuta Jumamosi mbele ya Mnyama Uwanja wa Taifa kwenye mchezo wa hatua ya 32 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports.
Licha ya Derald Mdamu kuanza kufunga bao dakika ya 34 halikudumu kwani Clatous Chama alisawazisha dakika ya 45+2 kabla ya Kahata kulipeperusha kabisa fuko la fedha kwa kufunga bao la ushindi dakika ya 84.
Habari kutoka ndani ya Mwadui zimeeleza kuwa wachezaji wote waliahidiwa kupewa kila mmoja laki moja iwapo wangeshinda mbele ya Simba.
“Wachezaji wote waliahidiwa kupewa laki moja iwapo wangeshinda mbele ya Simba, mezani kulikuwa na dau la milioni mbili hivyo kupoteza kwao kumepeperusha fuko la hela zote zilizowekwa mezani na wadau,” kilieleza chanzo.
Akifafanua ishu hiyo, Meneja wa Mwadui, David Chakala, alisema huwa ni kawaida kwao kutoa fungu la fedha kwa wachezaji wao ili kuwaongezea morali. “Tukiwa vizuri huwa tunatenga fungu la fedha ili kuongeza morali.
Lakini huwa tunawasisitiza wacheze kwa juhudi kwa kuwa ni kazi yao na wanajiweka wenyewe sokoni,” alisema Chakala ambaye aligoma kuzungumzia kama waliwatengea milioni 2 wachezaji wao katika mchezo dhidi ya Simba akidai hilo ni suala la ndani.
LUNYAMADZO MLYUKA, Dar es Salaam