×

Wakazi wa Mto wa Mbu Walia na Mafuriko

Watumishi wa kambi za utalii katika mji mdogo wa mto wa mbu wakihamisha mahema (TENT) kwenye kambi za watalii kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika eneo hilo ambalo inanadaiwa halina mifereji ya kutosha kuruhusu maji kupita hivyo kusababisha maji kutuama kwenye makazi, mashamba na kambi za wageni.
Zoezi likiendelea la kuhamisha mahema (TENT) kwenye kambi za watalii kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika eneo hilo.
Baadhi ya wananchi wakifyeka majani kwenye mitaro ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi.

Wakazi wa mji Mdogo wa Mto wa Mbu wilayani Monduli mkoani Arusha eneo la Migungani ‘A’ wameiomba serikali kunusuru maisha yao na hatari ya kusombwa na mafuriko kutokana na kukosekana miundombinu imara inayoruhusu maji ya mvua kutiririka  ambayo yamekuwa yakikosa muelekeo hivyo kutuama  katika makazi, shule na kusababisha hofu kubwa kwa maisha yao na hata kambi za watalii wanaolala eneo hilo kufurika maji.

 

Tangu mvua zimeanza kunyesha katika msimu huu wakazi hao wamekuwa wakikumbana na adha kubwa ya maji kujaa katika nyumba zao, mashamba, shule ambapo hali imezidi kuwa mbaya zaidi pale baadhi ya kambi za watalii nazo kuonekana kujaa maji hivyo kusababisha wageni kushindwa kulala katika eneo hilo.

 

Mmoja wa wakazi hao Catherine Kubena, anasema kukosekana kwa miundombinu rafiki ya mifereji ndiyo inachangia kusababisha mafuriko eneo hilo hivyo anaiomba serikali kunusuru wakazi hao kabla ya kuleta maafa makubwa kutokana na  mvua zinazoendelea kunyesha huenda zikaleta madhara zaidi.

 

“Yaani sasa hivi mvua ikinyesha watu hatuelewi tutoke nje au tubaki ndani maana maji yanajaa vitu vinaharibika hata hatulali usingizi kweli maisha yetu yapo hatarini tunaomba serikali iingilie kati suala hili kwa kutuongezea makalavati ili tuweze kuishi kwa amani”.

 

Ukosefu wa makalavati ya kutosha na mifereji ambayo inaonekana nyembamba ikishindwa kuhimili kiwango cha maji yanayotiririka lakini pia baadhi ikiwa imeziba  ndiyo  chanzo cha tatizo lote hilo, ambapo  wananchi hawa wanaamua kupaza sauti zao baada ya hali kuendelea kuwa mbaya.

 

Katika sekta ya utalii nayo ikionekana kuathirika zaidi ambapo baadhi ya maeneo yaliyoathirika zaidi ni kambi ya kulala wageni ambapo pamejaa mafuriko hivyo kusababisha wageni kushindwa kulala katika kambi hizo.

 

“Mifereji imeziba, mingine haina uwezo wa kupitisha maji hivi unavyoona hali ni mbaya sana harufu ya maji yamejaa kila mahali na tunahofia afya zetu huenda wakati wowote pakatokea mlipuko wa magonjwa ya tumbo maana mashimo ya vyoo yanazibuliwa kipindi hiki cha mvua.”alisema Janeth

 

Hata hivyo wakati wakisubiri msaada wa serikali wananchi hao wameamua kujiongeza kwa kujitolea kwa nguvu zao kuanza kuzibua mitaro ya maji lakini bado wanakabiliwa na  changamoto ya vitendea kazi duni.

Leave a Comment