×

Vigogo 6 wa Lugola Wafika TAKUKURU na Laptops Walizopewa Ulaya

WALIOKUWA wajumbe wa kamati ya utekelezaji wa makubaliano yaliyosainiwa Agosti 22, 2019, kati ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Kampuni ya Rom Solution Co. Ltd ya nchini Romania, wanaodaiwa kuingia mkataba wa hovyo na kupewa ‘laptops’ na posho za vikao na kampuni hiyo, leo Februari 5, 2020, wamefika katika ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambanana Rushwa (TAKUKURU) jijini Dodoma kuhojiwa kutokana na tuhuma zinazowakabili.

Vigogo hao sita ni miongoni mwa viongozi waliotajwa na Rais  John Magufuli kuwa walikuwa wakipatiwa posho za vikao kiasi cha dola 800 na laptop kwa kila kikao walichokifanya na kampuni hiyo nchini Romania kwa ajili ya makubaliano hayo.

Wajumbe hao ambao ni pamoja na Kamishna wa Zimamoto, Mbaraka Semwanza; Naibu Kamishna wa Zimamoto, Fikiri Salla;  Naibu Kamishna wa Zimamoto, Lusekelo Chaula;  Naibu Kamishna Zimamoto, Ully Mburuko;  Mchumi Zimamoto, Boniface Kipomela na Mchumi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Felis Mshana,  wamefika wakiwa na laptops  zinazodaiwa kuwa walipewa na kampuni hiyo wakati wa makubaliano hayo.

Aidha, wajumbe hao pia wanadaiwa kuwa walikuwa wakilipwa posho za vikao USD 800 na kampuni hiyo wakati wakiwa wanakutana katika vikao vyao vya majadiliano.

 

Sakata hilo la mkataba wa kununua vifaa vya Zimamoto vyenye thamani ya zaidi ya Tsh trilioni 1, limesababisha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola,  kuachishwa wadhifa huo.

Leave a Comment