×

Waziri Kairuki Kuwaongoza Watanzania Kwenda Indonesia,Thailand Na Singapore

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki.

 

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) wanaratibu ziara ya wawekezaji na wafanyabiashara wa Tanzania kwenda nchini Indonesia, Singapore na Thailand kwa lengo la kutafuta fursa za ushirikiano katika uwekezaji na biashara kupitia maeneo ya ubia, masoko na teknolojia.  Kiongozi wa msafara atakuwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki.
Katika ziara hiyo kutafanyika kongamano la siku moja kila nchi kati ya Tanzania na nchi husika (Indonesia, Thailand na Singapore) ili kuwakutanisha ana kwa ana wafanyabiashara/wawekezaji wa Tanzania na nchi hizo kisha kwa nia ya kujadiliana uwepo wa fursa mbalimbali za kibiashara na uwekezaji zinazoweza kuanzishwa na kuendelezwa katika sekta mbalimbali. Sekta lengwa ni viwanda, kilimo, ujenzi, mawasiliano, madawa na vifaa tiba, madini, fedha, utalii, TEHAMA na biashara kwa ujumla.
Ujumbe huo utaondoka nchini tarehe 23 Februari, 2020 na kushiriki  makongamano kama ifutavyo; Kongamano kati ya Tanzania na Indonesia ni tarehe 24 Februari 2020, Kongamano kati ya Tanzania na Thailand ni tarehe 26 Februari, 2020 na Kongamano kati ya Tanzania na Singapore ni tarehe 28 Februari, 2020.
Kila mshiriki atajigharamia usafiri, malazi na chakula. Tunakaribisha wadau wenye nia ya kushiriki katika ziara hii wajisajili kupitia TPSF kwa barua pepe [email protected] au simu +255 682 031 728/ +255 0784 323068.
Kwa mawasiliano zaidi; tembelea ofisi za TIC Makao Makuu zilizopo Dar es Salaam mtaa wa Shaaaban Robert, jirani na ofisi ndogo za Bunge au wasiliana na Benson Nkini kwa namba 0715923777 au Diana Ladislaus kwa namba 0719653079.

Leave a Comment