The House of Favourite Newspapers

Samatta Mzigoni Tena Leo Premier

0

MSHAMBULIAJI wa Aston Villa, Mtanzania, Mbwana Samatta anatarajia kuiongoza timu yake leo Jumamosi katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Southampton utakaopigwa kwenye Uwanja wa St Mary’s. Villa inashuka kwenye mchezo huo watakaopiga ugenini ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo uliopita kwa kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya Tottenham Hotspur.

 

Hii inakuwa ni mechi ya tatu kwa Samatta katika ligi kuu ya nchi hiyo tangu ajiunge na Villa kwa mkataba wa miaka minne na nusu akitokea KRC Genk ya Ubelgiji. Villa inapambana kujiokoa katika janga la kushuka daraja kutokana na kuwepo kwenye nafasi ya 17 ikiwa na pointi 25 baada ya kucheza mechi 26.

Championi limezungumza na baba mzazi wa mshambuliaji huyo, mzee Ally Samatta, alisema kuwa anaamini Villa watashinda mchezo wa leo Jumamosi baada ya matokeo mabaya ya mchezo uliopita.

 

“Nadhani watashinda hasa kutokana na matokeo ya mechi iliyopita kwa sababu hakuweza kufanya vizuri lakini naamini huwa nikiota timu yake inashinda huwa wanashinda kweli.

 

“Suala la kushuka daraja nadhani halitawakuta kwa sababu wamekuwa wakicheza vizuri tofauti na hata ya timu zile ambazo zimekuwa zikisifiwa zinacheza vizuri ingawa wamekuwa wakiangushwa na safu ya ulinzi,” alisema mzee Samatta

Leave A Reply