×

Wachina Wanaswa Wakitaka Kumpa Kamishna Mkuu TRA Mil. 11

JUZI Jumatatu, Feb. 24, 2020, mida ya saa 6 mchana, Kamishna Mkuu wa TRA, Dkt. Edwin Mhede, akiwa ofisini kwake  alipokea taarifa kutoka kwa watumishi mwenzake (si wa mamlaka hiyo) ila mtumishi wa umma, akimueleza kulikuwa  na wateja waliotaka kumuona kuhusu masuala ya kodi wakidai walikadiriwa kodi kubwa kuliko ilivyopaswa, hivyo waliomba kuonana naye ili waweze kumweleza jambo hilo.

 

Kwa mujibu wa Mhede, alipokutana na wateja hao, walitoa karatasi ambazo zilionyesha zinahitaji ufafanuzi wa Kamishna Mkuu.

 

Kamishna huyo anadai kuwa alishaweka sera ya kutokufanya kazi peke yake lazima awe na wasaidizi wake, hivyo wakati wageni hao wakiendelea kutoa maelezo wakatoa kibunda cha fedha za Kimarekani, na Kamishna hakujua ni kiasi gani.

 

“Hapo kwa kweli ilinitoa kwenye reli nikaona hiki ni kitu ambacho sio cha kawaida.  Nikawauliza kwa nini mnafanya hivyo,  wakadai wananipa tu kama zawadi,” alisema kamishna huyo.

 

Baada ya hapo alimwambia msaidizi wake ahesabu hizo fedha na zikawa ni dola 5,000 (zaidi ya Tsh milioni 11.5) akazikataa na hatua alizochukua ni kuwaambia waandike maelezo nao wakaandika kuwa walitaka kumpa fedha kamishna mkuu akazikataa mbele ya shahidi ambaye ni msaidizi wake.

 

Kamishna aliamua kuwachunguza ili ajue ni kina nani,  akagundua  ni wamiliki wa kampuni inayoitwa Rong Lan International Industry and Trade Company Limited ambayo ipo Mafinga mkoani Iringa na kwenye taarifa za TRA zilionyesha walikuwa wamekaguliwa muda mfupi na kukutwa na hatia ya kukwepa kodi kiasi cha shilingi bilioni 1.735 na nyaraka anazo kamishna huyo.

 

Pia muda wa kulipa au kukomboa kodi ulikuwa umeisha tangu 21/02/2020 na kamishna alikuwa keshatoa maagizo kwa watu husika kuwa ni lazima wakomboe kodi na alitoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili taratibu za kisheria ziweze kuchukuliwa na mamlaka husika.

 

Aidha, kamishna huyo alimaliza kwa kutoa rai kwa watu wote kutodiriki kutoa rushwa kwani  hawashawishiki na wapo kusimamia sheria na hawataingia kwenye ulafi wa fedha haramu.

 

Leave a Comment