×

Mahakama Yakubali Maombi ya Rugemalira

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imekubali kupokea hoja za maombi ya mfanyabiashara James Rugemalira anayetaka kuondolewa kwenye kesi ya utakatishaji fedha wa Sh. bil 309.4.

 

Hatua hiyo imekuja wakati shauri hilo lilipoitishwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

 

Wakili wa utetezi, John Chuma amedai kuwa mteja wake ameshawasilisha hoja za pingamizi la awali lakini hajapata majibu yoyote kutoka upande wa Jamhuri.

 

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, amedai baadhi ya nyaraka amezipata leo mahakamani hapo na kuwa upande wa Jamhuri upo tayari kusikiliza hoja hizo kwa njia ya mdomo kama nyaraka hizo zimeshaingizwa kwenye kumbukumbu ya mahakama hata kwa wakati huo kama ratiba ingeruhusu.

 

Wankyo amedai mshtakiwa wa pili amekua anajiwasilisha mwenyewe huku akiwa na uwakilishi wa mawakili hivyo anapaswa kusema kama amewaacha ama wanaendelea.

 

Akijibu suala hilo, Rugemarila amedai kuwa amekuwa na wawakilishi hata zaidi ya thelathini lakini kuna hoja lazima aziwasilishe mwenyewe na kuwa hilo jambo walitakiwa kulalamika mawakili wake na si  yeye kwani sheria inamruhusu kujiwakilisha.

 

Baada ya hoja hizo, Hakimu Shaidi ameahirisha shauri hilo hadi Machi 12, 2020 litakapokuja kutajwa na upande wa Jamhuri kuwasilisha majibu.

 

Mbali na Rugemalira, washitakiwa wengine ni mmiliki wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power (IPTL) na Mwanasheria wa IPTL, Joseph Makandege.

 

Washitakiwa Seth na Rugemalira kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27

Leave a Comment