IKIWA ni muda mfupi baada ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli, kuazimia kumfukuza uanachama aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi, Bernard Membe, kwa kukiuka maadili ya chama, naye ametoa kauli yake.
Membe ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Mtama na kuingia katika kinyang’yiro cha kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015, kupitia akaunti yake ya Twitter amesema:
“Watanzania wenzangu nimepata habari ya kufukuzwa kwangu kutoka kwenye Chama changu cha CCM. Simu zinamiminika hadi nashindwa kuzijibu. Tulieni! Nitapata muda wa kuongea na wote muda si mrefu!”
Katika kikao hicho, Katibu Mkuu Mstaafu wa chama hicho Yusuf Makamba, amesamehewa kutokana na kuomba kusamehewa makosa aliyokuwa akidaiwa kuyatenda ya kwenda kinyume na maadili ya chama hicho.
Aidha, Katibu Mkuu Mstaafu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, amepewa adhabu ya karipio kali kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili ya chama hicho na atakuwa kwenye uangalizi kwa kipindi cha miezi 18.
