×

Tshishimbi Amaliza Utata Wa Morrison, Luis

BAADA ya ubishani mkubwa wa kupambanishwa kati ya kiungo wa Yanga, Bernard Morrison na yule wa Simba, Luis Miquissone, hatimaye kiungo mkabaji, Mkongomani, Papy Tshishimbi, ameibuka na kumaliza utata kwa mashabiki wa timu hizo kongwe.

 

Hiyo ni baada ya viungo hao wawili kupambanishwa na mashabiki wa timu hiyo kwenye michezo iliyopita ya Ligi Kuu Bara na Kombe la FA waliyozichezea timu zao.

Morrison tangu amejiunga na Yanga amecheza michezo saba akipiga asisti tatu huku akifunga mabao mawili pekee na Luis amecheza mechi nne akifunga bao moja na kupiga asisti moja pekee.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Tshishimbi alisema kuwa, wachezaji hao wote wana viwango sawa, kikubwa kila mmoja anaisaidia timu yake kupata matokeo hicho ndiyo cha msingi.

 

Tshishimbi ambaye ni nahodha wa Yanga, alisema kuwa utofauti utakuja kutokea Morrison akienda kucheza Simba na Luis akicheza Yanga wote hawataonekana wazuri kwa sababu wanaenda kukutana na wachezaji wazuri ambao bado hawajazoeana nao.

Aliongeza kuwa, wachezaji hao wote wanaonekana bora katika timu zao kutokana na kukaa pamoja na kuzoeana hivyo huwa rahisi kwao kung’aa.

 

“Ninafahamu wachezaji Morrison na Luis wanavyoshindanishwa na mashabiki wa timu hizi za Simba na Yanga, hiyo inaonyesha kuwa wachezaji hao ni bora ndiyo sababu ya kupambanishwa.

 

“Nikiri uwezo wa wachezaji wote kuwa ni wazuri kutokana na kuzipambania timu zao na kupata matokeo mazuri, hilo ndilo jambo la muhimu lakini hao wanaonekana bora kutokana na kukaa pamoja na kuzoeana huku wakijua mipira ya aina gani wanayoweza kucheza.

 

“Nikiwa na maana kuwa, ni ngumu Morrison kung’aa akiwa Simba kwa kuwa kila mchezaji hapa Yanga, tayari ameshajua ampigie mpira wa aina gani ili aweze kucheza soka safi la kuvutia na ndivyo itakavyokuwa kwa Luis, ni ngumu kung’aa akiwa Yanga kwani yeye tayari wameshajua wachezaji wenzake anapenda apigiwe pasi za aina gani.

 

“Lakini ukweli ni kwamba wachezaji wote ni wazuri kila mmoja anaipambania timu yake kupata matokeo mazuri tofauti na mbwembwe na vionjo vya kuuchezea mpira wanavyovitoa uwanjani,” alisema Tshishimbi.

Leave a Comment