×

Nandy Atoboa Siri ya Kusainiwa Wasafi

KWA mara ya kwanza, malkia wa Bongo Fleva, Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’ amefunguka juu ya zile tetesi za kusainiwa kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) chini ya mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

 

Mwishoni mwa mwaka jana, zilisambaa tetesi nyingi mitandaoni kuwa mwanadada huyo yupo njiani kuchukuliwa na Wasafi, lakini hakuwahi kueleza ukweli wa ishu hiyo.

Nandy ameliambia Gazeti la IJUMAA WIKIENDA kwamba, hajutii kwa lolote kutokusainiwa kwenye lebo hiyo kubwa ya muziki.

 

Nandy alisema, alikuwa sehemu ya timu ya Wasafi mwanzoni kabisa, lakini hakusainiwa kwenye lebo hiyo chini ya mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Nandy alisema, aliondoka Wasafi baada ya kuteuliwa kwenda kwenye shindano la uimbaji lililokwenda kwa jina la Tecno Own The Stage nchini Nigeria ambapo aliibuka mshindi.

 

Alisema, baada ya kurejea Tanzania, alikwenda kujiunga kwenye jumba la kukuza vipaji la THT (Tanzania House of Talent) kabla ya kuwa solo artist (msanii anayejitegemea).

Nandy alisema hajutii kutosainiwa Wasafi kwa sababu yupo juu na anafanya vizuri kwenye fani yake hiyo.

 

“Sijawahi kusainiwa na Wasafi, lakini nilikuwa Wasafi mwanzoni, nikaenda Tecno Own The Stage, niliporudi nikaingia THT.

 

“Sijutii kwa sababu wote tunafanya vizuri. Wasafi wanafanya vizuri na mimi ninafanya vizuri nikiwa mwenyewe,” alisema Nandy aliyeachia ngoma yake mpya ya Na Nusu, inayotrendi kwenye YouTube kwa sasa.

Aliweka sawa, hakuwahi kupanga kusajiliwa Wasafi, lakini tetesi hizo ziliibuka baada ya kunaswa na Diamond au Mondi walipokuwa Dubai kikazi.

STORI: IMELDA MTEMA, DAR

Leave a Comment