×

Kagere Apewa Silaha Zote Za Kuwaua Yanga

MBELGIJI wa Simba, Sven Vandenbroeck amefunguka kuwa straika wake, Meddie Kagere ataanza katika mechi yao dhidi ya Yanga, keshokutwa Jumapili kwa kuwa yuko sawa na alipumzika kwa muda katika mchezo uliopita juzi dhidi ya Azam FC kwa sababu maalum.

 

Sven ameweka wazi kwamba aliamua kumuweka benchi Kagere katika mechi ya juzi kisha kuingia katika dakika ya 61 akichukua nafasi ya Deo Kanda, sababu kubwa ni kumfanya awe fiti kwa mchezo wa Jumapili akiamini atakuwa na msaada mkubwa katika kipute hicho.

Mara baada ya kuingia akitokea benchi juzi, Kagere ambaye anaongoza kwa mabao msimu huu alifunga bao moja kati ya matatu ya Simba huku Azam FC wakipata mawili.

 

Sven ameliambia Championi Ijumaa, kuwa Kagere ataanza kwenye mechi hiyo kwa sababu yuko sawa kwa sasa baada ya kuwa na majeraha ya enka aliyoumia katika mechi yao dhidi ya Stand United katika Kombe la Shirikisho (FA).

“Tulicheza kule Shinyanga kwenye FA, ndipo Kagere akapata majeraha kidogo ndiyo maana kwenye mechi na Azam FC alianza nje, lakini bado akaingia na kufunga.

 

“Nina furaha kuona aliingia na kufunga na amefunga bao baada ya mechi kadhaa kutofunga huko nyuma. Subiri kuona akianza katika mechi ijayo Jumapili,” alisema Sven.

Stori: Said Ally, Dar es Salaam

Leave a Comment