×

Bao la Morrison Lamvuruga Mbelgiji

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael amelisifu bao la kiungo mshambuliaji wake, Mghana Bernard Morrison, na anaamini asingejitonesha na kumtoa uwanjani, basi angewafunga bao lingine la pili katika mchezo huo.

 

Kauli ya kocha huyo imekuja baada ya Yanga kuitungua Simba bao 1-0 mfungaji akiwa ni Morrison katika dakika ya 43 kwa njia ya faulo ya umbali wa mita 18. Mchezo huo wa watani wa jadi nchini Tanzania ulikuwa wa kwanza kwa Mghana huyo na kocha wake.

 

Akizungumza na Gazeti la Championi Jumatano, Luc alisema kuwa Morrison alipata majeraha ya goti mazoezini siku tatu kabla ya mchezo huo wa Kariakoo Derby, lakini hawakuweka wazi katika hilo kwa kuhofia kuvujisha mbinu kwa mpinzani wao.

Luc alisema hakutaka kumtumia kiungo huyo, lakini baada ya yeye mwenyewe kuomba acheze dakika 45 ndiyo akampanga katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo. Aliongeza kuwa alimpanga baada ya kumuahidi kuifunga Simba katika dakika 45 alizoomba kucheza na kufanikiwa kutimiza hilo kwa kufunga katika dakika ya 43 ya mchezo huo.

 

“Morrison hakuwepo kwenye mipango yangu ya kumtumia katika kikosi cha kwanza, ni baada ya kupata majeraha siku tatu kabla ya mchezo huo, nilimpanga baada ya yeye mwenyewe kuomba acheze dakika 45 tu. “Na ndiyo maana alivyoongeza dakika alionekana kusikia maumivu na kuangukaanguka kila wakati kabla ya kumtoa dakika ya 50 na kumuingiza Sibomana (Patrick). “Mabadiliko ya Morrison niliyajua muda mrefu hivyo nilikuwa nimeshajiandaa kabisa, ninaamini kama asingekuwa na majeraha basi angefunga mabao zaidi ya hilo moja, kwani ninafahamu uwezo wake,” alisema Luc.

 

Leave a Comment