JESHI la Magereza nchini limesema kauli zilizotolewa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) walipotoka gerezani si za kweli na kwamba mambo wanayodai kufanyiwa ni utaratibu wa kawaida kwa wafungwa na mahabusu.
Akizungumza na wanahabari jijini Dodoma msemaji Mkuu wa Jeshi la Magereza Mrakibu Mwandamizi, Amina Kavilondo, amezitaja kauli hizo kuwa ni pamoja na mateso ndani ya magereza ambapo wafungwa wanaishi kama wanyama na kutokuwa na haki pamoja na madai ya kupimwa ukimwi hadharani.
“Taratibu zilizofanywa dhidi yao ni za kawaida na hazijafanywa kwa kuwa wao ni viongozi wa Chadema ila vimefanywa kwa mujibu wa taratibu za Magereza na vinafanywa kwa kila mfungwa sio kwao pekee,” amesema.
Akizungumzia suala la afya na ukaguzi, amesema kuwa jukumu la Magereza ni kuhakikisha usalama wa mfungwa na endapo atakutwa na tatizo atakuwa chini ya uangalizi zaidi kuliko wengine.
“Hao ni viongozi watumie nafasi zao wanapopita katika Magereza kufanya ukaguzi na kuzungumzia changamoto hizo ambapo zitapatiwa ufumbuzi kuliko kusubiri mpaka wawe wafungwa ndipo watoe kauli hizo,” amesema.
Pia amezungumzia kuhusu ukaguzi maalum unaofanywa kabla ya kuingia gerezani kwa kutumia mashine za ukaguzi, mfungwa kupewa shughuli mbalimbali kama kufanya usafi na nyingine, kupigwa kwa virungu kwa mahabusu na tarehe ya mahabusu kupelekwa mahakamani huku wakidai kuwa mkuu wa jeshi kukiri kuwa hatoshi kwenye nafasi hiyo.
Amelitolea ufafanuzi ambapo amesema, kauli hizo haziko sahihi na zinalenga kupotosha utendaji kazi wa jeshi la Magereza nchini.
