KIONGOZI Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ameishauri serikali mambo matatu ambayo itatakiwa kufanya ili kuokoa uchumi wa nchi katika mazingira ya sasa ya kusambaa duniani hadi nchini kwa homa inayotokana na virusi vya Corona.
Taarifa iliyotolewa na chama hicho Machi 17, 2020, kwa umma, kupitia kwake inasema:
#COVID19TZA Serikali imethibitisha uwepo wa virusi vya Corona Tanzania. Utulivu ni muhimu kwani kukiwa na maandalizi ya kutosha tunaweza kukabili madhara ya mlipuko huu. Nashauri mambo 3 muhimu sana, kwa maoni yangu.
Tunaona nchi nyingine kukiwa na ‘panic’ ya chakula. Watu wetu ni fukara sana, bei za chakula zitapanda na wengi hawatamudu.
Pia serikali haina akiba ya kutosha ya chakula kwenye ghala la taifa. Kuna nafaka ya kutosha siku 3 tu kwa kila Mtanzania. Ni vema Serikali kufanya uamuzi wa haraka kununua chakula ili kukigawa maeneo itakapohitajika.
Tanzania inategemea sekta ya utalii kwa kiasi kikubwa katika mapato ya fedha za kigeni na ajira kwa raia wake. Mlipuko huu unaathiri sana sekta hii ambayo inaingizia taifa wastani wa Dola za Marekani 2.5 bilioni kwa mwaka sawa na 25% ya mapato yote ya fedha za kigeni yanayoingia nchini.
Naishauri serikali kukutana na wafanyabiashara wote kwenye sekta ya utalii na vyama vya wafanyakazi kwenye sekta hiyo kwa lengo la kupata tathmini ya pamoja ya madhara ya mlipuko huu kwa sekta ya utalii na huduma zake.
Serikali itazame namna ya kuwafidia ( stimulus package) wafanyabiashara katika sekta hiyo ili kulinda ajira za wananchi. Ikiwezekana fidia iwe ni kulinda ajira kwa kufidia gharama za wafanyakazi ( payroll costs).
Waziri wa Fedha na Uchumi apeleke bungeni taarifa ya utafiti wa madhara ya mlipuko wa Corona kwa uchumi wa Tanzania kwa ujumla na bunge lijadili kwa maslahi ya taifa ili kutoa mapendekezo ya kibajeti kuhami uchumi wa nchi yetu na hasa kulinda biashara ndogo, wafanyakazi kwenye sekta zilizo hatarini kama utalii, huduma za vyakula, usafirishaji na uchuuzi.
Zitto Kabwe, MP
Kiongozi wa Chama
ACT Wazalendo
17/3/2020
