×

Maajabu! Mtoto Alivyonusurika Ajali ya Moto wa Gesi

 

HAKIKA Mungu ni mwema, ndivyo unavyoweza kutafsiri baada ya mtoto Ayubu Mohamed (2) aliyekuwa ameuchapa usingizi kunusurika na kifo baada ya rundo la mitungi ya gesi kulipuka na kuunguza vibaya nyumba aliyokuwa amelala.

 

Hata hivyo, mtoto huyo ameungua mkono wa kulia katika ajali hiyo ambayo imewajeruhi waandishi wanne waliokuwa wakichukua taarifa za tukio hilo.

Waandishi hao ni Omary Husein (Star tv), Nicholaus Mwanabarusi (Global Tv), Salum Yusufu (Abood Media) na Hassan Niga (Tv Imani).

 

Tukio hilo lililotokea Machi 14 mwaka huu katika nyumba iliyopo Mtaa wa Mafisa Mzambarauni Kata ya Mwembesongo Mkoani Morogoro, limetokea mtaa wa pili ilipotokea ajali mbaya ya mlipuko wa lori la mafuta iliyotokea Agosti 10 mwaka jana na kuuwa watu zaidi ya 100.

MAMA AMUOKOA MTOTO KIMAFIA

Baada ya kutokea kwa tukio hilo, RISASI lilitinga haraka katika eneo la tukio na kushuhudia mtoto huyo akiopolewa kwenye moto huo na kukimbizwa hospitali kwa usafiri wa bodaboda.

 

Akiwa juu ya bodaboda hiyo, Mama mzazi wa mtoto huyo, Zainabu Mussa alisema “Mungu ni mwema, nyumba tunayoishi ni ‘changanyikeni’ kwa maana ya wapangaji wengi akiwemo kijana anayefahamika kwa jina la Singo ambaye chumbani kwake alikuwa akihifadhi mitungi ya gesi.

 

“Kila siku muda wa mchana, mwanangu huwa analala chumbani, ni chumba kilichopo jirani na chumba ambacho mitungi hiyo imelipuka.

 

“Muda huo wakati mwanangu kalala, nilikuwa nje nafua nguo, nilisikia mlipuko wa mitungi ya gesi, ghafla moto ukawaka, nikajitosa kwenye moto na kumchomoa mwanangu ambaye katika tukio hilo ameungua mkono na muda huu tunamkimbiza hospitali.

 

“Kwenye chumba chetu vitu vyote vimeungua, hatukutoa hata kijiko, akili yangu na mume wangu Mohamed Rashid ilikuwa ni kumuokoa mtoto wetu, vitu vinatafutwa” alisema Mama huyo.

 

Wakizungumza na RISASI baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo akiwamo dereva wa bodaboda aliyefahamika kwa jina la Ninga Uwezo ambaye pia ni mlinda mlango wa timu ya Burkinafaso yenye maskani yake Mafisa alisema;

“Mungu ni mkubwa, waandishi wa habari walikuwa nje ya nyumba wameungua vibaya, huyu mtoto aliyekuwa amelala ndani kanusurika ingawa kaungua kidogo mkononi.”

Aidha, Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa huo Mohamed Mayowela aliyekuwepo eneo la tukio, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo mtaani kwake.

 

Hata hivyo, Mayowela alisema mmiliki wa nyumba hiyo amefariki, hivyo wanaishi wapangaji waliopangishwa na watoto wa marehemu ambao wengi wao hawaishi kwenye nyumba hiyo.

 

“Kuhusu mmiliki wa mitungi, nimeambiwa kwamba haishi kwenye mtaa huu ingawa chumba hiki alipanga yeye na kumuweka kijana aliyetajwa kwa jina moja la Singo. Wapangaji wanadai chumba hicho kilijaa mitungi hiyo ya gesi iliyokuwa inauzwa kwa siri nyakati za usiku” alisema.

 

STORI: Dustan Shekidele, Morogoro

Leave a Comment