LIGI Kuu Tanzania Bara kwa sasa imesimama, Tanzania tumeungana na zaidi ya mataifa 170 kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona ambavyo ni hatari, hasa pale kinga ya mwili inapokuwa imeshuka. Basi ni wajibu wa kila mmoja kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ili kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo ambavyo kitaalamu vinaitwa Covid-19.
Medani ya michezo hivi sasa dunia nzima imesimama, siyo Ulaya wala Tanzania lakini hilo haliwezi kutufanya tusiijadili michezo yenyewe, hapa Tanzania kuna timu inaitwa Kagera Sugar timu hii tangu ipande daraja miaka ya 2004 kucheza ligi kuu haijashuka daraja mpaka leo, ndiyo timu pekee ambayo inawafanya wachezaji wake waishi kifalme zaidi tofauti na timu nyingine kwenye ligi, jambo ambalo linawafanya wachezaji wa timu nyingine kujituma ili waweze kupata kazi kwenye timu hiyo yenye maskani yake wilayani Misenyi mkoani Kagera.
Timu hiyo msimu wa 2018/19 nusura ishuke daraja pale ambapo ilijikuta ikicheza michezo ya ‘Play off’ na ilikutana na Pamba ya Mwanza. Walicheza michezo miwili, wa kwanza kwenye Uwanja wa Nyamagana uliomalizika kwa suluhu na wa pili Kagera Sugar wakaifunga Pamba mabao 2-0 Kaitaba. Lakini baada ya kuanza kwa msimu huu timu hiyo ilianza kwa moto wa aina yake.
Iliwashangaza wengi, walistaajabu kuona Kagera ikianza msimu kwa ushindani wa hali ya juu chini ya kocha Mecky Maxime ambaye ni nahodha wa zamani wa timu ya taifa na kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar ya Morogoro. Kocha huyo alikisuka vilivyo kikosi chake, vijana kama Awesu Awesu, Ramadhan Kagawa, Zawadi Mauya na Abdallah Seseme, waliifanya safu ya kiungo ya Kagera Sugar kuwa tishio.
Waliweza kuitawala safu hiyo ya kiungo kwa kila timu waliyocheza nayo. Katika safu ya ushambuliaji, nyota wawili wa zamani wa Yanga Yusuf Mhilu na Geoffrey Mwashiuya pamoja na nyota wa zamani wa Mbao, Evaristus Mjwahuki ambaye baadaye alipata majeraha, walianza kwa moto. Walikuwa hatari, hakika Kagera ilivutia kuitazama baada ya raundi 12 za mwanzo.
Kagera ilikuwa imejikita katika nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Ilifurahisha sana na iliaminika kwamba huenda msimu huu itashindana katika nafasi hizo za juu, lakini hivi sasa mambo hayako hivyo, kuna mdudu gani kaingia? Kwa sasa Kagera inapitia katika kipindi kigumu mno, mambo yamewageukia. Katika mechi 10 za mwisho, Kagera imeshinda mbili tu, imepoteza michezo sita na sare mbili. Iko nafasi ya 8 kwenye msimamo wa ligi baada ya michezo 29 na kujikusanyia pointi 41. Kagera Sugar imeyumba vilivyo.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, unaweza usione kama wako pabaya lakini mwenendo wao hivi karibuni unawaweka katika eneo la hofu, hivi sasa wanaiwaza playoff ya mwaka jana ambapo walipenya kwenye tundu la sindano baada ya kuifunga Pamba ya Mwanza.
Kwa sasa wako katika nafasi ya nane na alama 41. Ni alama nane tu juu ya eneo la kushuka daraja. Siyo ishara nzuri katika mechi hizi tisa za mwisho ambazo Kagera Sugar wamebakiwa nazo. Kocha mkuu wa kikosi hicho, Mecky Maxime, mwenyeji wa Morogoro, anapaswa kufanya jambo la kuhakikisha Kagera Sugar walau inacheza kwa kiwango bora na iepuke presha za kucheza michezo ya mtoano kwani kwa taarifa ambazo gazeti hili limezipata ni kwamba wachezaji wa timu hiyo, ndio wachezaji wanaoishi kifahari zaidi ya timu nyingi ukiondoa Simba, Azam na Yanga, kwa kuwa wachezaji hao wanalipwa posho ya shilingi elfu mbili kila siku wakienda kufanya mazoezi, wakienda safari hulipwa posho zaidi ya shilingi elfu thelathini kwa siku, wakishinda ndio usiseme. Kwa nini wanashindwa kutambua thamani ya Kagera Sugar mpaka idhalilike kiasi hiki?
Umefika wakati sasa Maxime afanye mapinduzi ya kifikra kwa wachezaji wake kwa kuwa ukiziondoa Simba na Yanga na Azam ,Kagera Sugar ndio timu pekee inayowajali wachezaji wake, mfano mchezaji Evarist Mjwahuki aliugua goti na klabu hiyo ilimgharamia matibabu ya upasuaji katika Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Moi), hivyo na wachezaji watambue thamani wanayopewa na Kagera ni kubwa, wanapaswa kurudisha fadhila na kwa kuwa michezo hii ya mwisho wa ligi huwa migumu kupitiliza, Kagera wanatakiwa kushinda michezo zaidi ya mitano ili wajiweke katika mazingira mazuri kwenye msimamo ili waweze kuepuka kucheza playoff tena, kwa kuwa kwa msimu uliopita, licha ya timu ya Pamba waliyocheza nayo kwenye playoff kuwa na wachezaji wachanga, Kagera walishalichungulia shimo la kutokea.
JOHNSON JAMES, MWANZA
