×

Mondi, Amina wa Kiba Gumzo Mjini

MJI mzito huu! Baada ya mapichapicha ya staa wa Bongo Fleva, Ali Salehe Kiba ‘King Kiba’ na mwanamitindo Hamisa Mobeto kuenea kila kona mtandaoni wakijiachia live kimahaba, mazito yameibuka.  Ghafla tu upepo umebadilika na sasa gumzo limekuwa ni kwa mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au ‘Mondi’ na mke wa Kiba, Amina Khaleef.

NINI KIMETOKEA?

Picha za Kiba na Mobeto ‘zilitrendi’ hatari kwenye mitandao ya kijamii baada ya wawili hao kushuti pamoja video ya Wimbo wa Dodo ambao ulikamata namba moja mara baada tu ya kuuachia kwenye Mtandao wa YouTube katikati ya wiki iliyopita.

Picha hizo za lokesheni ziliibua mengi ambapo wapo waliosema kuwa, wawili hao walilala pamoja hotelini huko Zanzibar, jambo ambalo lilimuibua Kiba na kukiri kulala hoteli moja na mrembo huyo kikazi huku akitoa ufafanuzi jinsi walivyofahamiana kwa muda mrefu.

Kiba alisema anamfahamu Mobeto siku nyingi kabla hata hawajawa mastaa na kwamba ni mtu anayemkubali, wanayeheshimiana na ndiyo maana alipofikiria mtu wa kuwa video vixen kwenye wimbo huo, Mobeto ndilo jina la kwanza lililomjia kichwani na aliona anafaa zaidi.

MONDI, AMINA GUMZO

Kitendo cha picha hizo ambazo zilionekana ni za kimahaba zaidi kusambaa, kiliibua gumzo kama lote huko Instagram na watu ambao walikuwa wanaunganishwa kwenye mchapo huo ni Amina wa Kiba na Mondi ambaye ni mzazi mwenza wa Mobeto. Wamezaa mtoto mmoja wa kiume aitwaye Dyllan.

Maoni mbalimbali yalitolewa kwenye mitandao ya kijamii, hususan Instagram kuhusu picha hizo ambapo watu wengi walieleza hisia na mitazamo yao kwa jinsi ambavyo Mondi na Amina wanavyoweza kulipokea suala hilo.

Maisha ya ndoa! Check out stunning photos of Ali Kiba's wife Amina

Kuna watu walipitiliza kimawazo kwa kusema, Mondi naye akitaka kiki inoge, basi naye ahakikishe anafanya kazi moja na mke wa Kiba ili tu kumjibu mpinzani wake huyo wa kimuziki.

Waliojiongeza hivyo walikuwa na hoja kwamba inawezekana jambo hilo likafanikiwa kwani Kiba na mkewe hawakuwa kwenye uhusiano mzuri, lakini hata hivyo, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA linafahamu, wanandoa hao kweli walikuwa kwenye tofauti, lakini walishazimaliza na sasa mapenzi ni motomoto.

IJUMAA WIKIENDA LAKUSANYA MAONI

Kinasa sauti cha Gazeti la IJUMAA WIKIENDA kilipoona suala hilo ndilo habari ya mjini, kilipita kwenye mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar na kukusanya maoni ya mashabiki wa mastaa hao.

“Kwa kweli hapa nashindwa kuelewa Mondi atakuwa anajisikiaje? Hivi Kiba alikosa video vixen wote waliojaa mjini hadi amfuate Mobeto ambaye anajua wazi kwamba amezaa na mpinzani wake, Diamond?” Alihoji Emma Charles, mkazi wa Kinondoni, Dar ambapo hoja hiyo iliungwa mkono na wengine wengi waliohojiwa.

WENGINE WAMTAJA AMINA

Naye Suzy wa Buguruni jijini Dar, alitoa maoni yaliyomtaja Amina ambayo pia yaliungwa mkono na watu wengi waliohojiwa. Alisema anashindwa kuelewa mke wa Kiba amezipokeaje picha hizo kwani zinaonekana kabisa walipata muda wa kutosha wa kujiachia.

“Kwa kweli Amina huko aliko najua atakuwa roho juu, hata kama alimruhusu Kiba afanye kazi na Mobeto, lakini sidhani kama anaweza kufurahia kuona picha za faragha kiasi kile na mumewe kukiri kabisa kwamba walilala hoteli moja kule Zanzibar,” alisema.

MAKABURI YAFUFULIWA

Akizungumza na IJUMAA WIKIENDA, mchambuzi wa habari za burudani Bongo, Erick Evarist alieleza jinsi ambavyo watu wamewajadili zaidi Mondi na Amina katika kipindi hiki.

“Unajua iko hivi, watu wamewataja zaidi Mondi na Amina kutokana na mitazamo inayotokana na historia za mahasimu hawa wawili. “Kuna baadhi ya mabinti ambao Mondi alikuwa nao karibu, Kiba naye akaja kuwa nao hivyo watu kuona kama wanashindana.

“Si unakumbuka Wolper alikuwa karibu na Kiba, baadaye Mondi naye akawa karibu naye. Kuna kipindi Mondi alikuwa karibu na Wema Sepetu, Kiba naye akafanya hivyo. Pia ilitokea kwa Tanasha, alianza kuwa karibu na Kiba, akafanya naye video ndipo Mondi naye alipokuja kuwa naye tena si tu ukaribu, bali wakawa wapenzi kabisa,” alisema Evarist.

Aidha, Evarist alisema, ndiyo maana hata baadhi ya watu sasa hivi wanajiongeza kwa kusema kwamba ili Mondi naye ajibu mapigo na awe juu kimuziki, afanye ngoma na Amina wa Kiba.

“Hizi timu ni shida sana, yaani wao sasa hivi wanawaza hata Mondi afanye kazi na Amina au hata mwanamke mwingine ambaye aliwahi kuwa na ukaribu na Kiba ilimradi tu kujibu mapigo.”

TUJIKUMBUSHE

Bifu la Kiba na Mondi ni la muda mrefu. Inaaminika chanzo chake ni Mondi kumfuta Kiba kwenye wimbo ambao ilikuwa watoe pamoja.

Mara kadhaa, Mondi amekuwa akijishusha na kusema yupo tayari kumaliza tofauti zao, lakini kwa Kiba imekuwa ishu nzito!

STORI: MWANDISHI WETU, DAR

Leave a Comment