NAOMBA nikiri wazi kwamba mimi ni Mkristo, nimeokoka na ninampenda Yesu ambaye siku zote amekuwa mwanga na kiongozi wa maisha yangu. Nasali sana, hakuna ninachokifanya bila kumwomba Mungu, huwa nasema yeye ni mshirika katika shughuli zangu zote.
Lakini pamoja na imani yangu hii siku zote nimeamini imani bila matendo ni sawasawa na bure, nasali, lakini nyuma ya sala zangu siku zote huwa naweka vitendo.
Imeandikwa katika maandiko matakatifu Kitabu cha Yakobo 2:14 kwamba: “Kuna faida gani, ndugu zangu, ikiwa mtu atasema ninayo imani na huku hana matendo?” neno hili linatuonesha kabisa kwamba imani peke yake haitoshi, ili izae matunda katika maisha yetu ni lazima iambatane na matendo.
Na kuna wakati nimejifunza kwamba yapo mambo ambayo yanahitaji matendo tu ili yatokee, hata kama imani haijahusika! Mfano mimi ninaweza kuwa na imani kwamba Mungu wangu anaweza kuzima taa ya umeme ndani ya nyumba yangu, jambo hili kweli Mungu wetu anaweza kulitenda, sina mashaka hata kidogo.
Kwa sababu ya imani yangu nitaanza kusali, ama kufunga kabisa siku tatu bila kula wala kunywa ili taa izime, haitazima! Lakini hapohapo atakuja mtu mwingine asiyeamini kabisa katika Mungu wangu, ameambiwa tu kwamba ili uzime taa kuna swichi ukutani, ataibonyeza na taa itazimika. Hapa kilichotumika ni matendo sio imani.
Mungu wa mbinguni aliwapa watu wake akili, hekima na maarifa ili waweze kutafuta suluhisho la matatizo yao, mwisho wa siku kazi zote hizo anayezifanya ni yeye kupitia kwa watu wake. Aliyetengeneza swichi ya umeme na umeme wenyewe ni Mungu kupitia kwa mtu aitwaye Thomas Edson lengo lake likiwa ni kuwahudumia watu aliowaumba.
Hakuna ubaya katika kuwa na imani, tatizo pekee huanzia pale ambapo imani inatawala halafu kunakuwa na upungufu ama ukosefu wa matendo, hakika tutaendelea kuonesha kwamba imani zetu hazina nguvu, wakati Mungu mwenyewe ametuagiza kwamba imani zetu siku zote ziambatane na matendo, ndiyo maana katika kitabu hichohicho cha Yakobo 2:17 Biblia inasema “Imani peke yake kama haina matendo imekufa.”
Kwa nini nimeamua kuyasema maneno haya leo? Ndugu zangu, taifa letu na ulimwengu mzima linapita katika wakati mgumu kabisa wa gonjwa hatari la Covid 19. Watu wengi wamepoteza maisha na maelfu wanazidi kuambukizwa, hofu imeikamata dunia hakuna mwenye uhakika wa kupona.
Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Magufuli alilitangazia taifa kwamba kuanzia Aprili 17-19, Watanzania tuzitumie siku hizo kumwomba Mungu wetu atuepushe na balaa hili.
Hakuna kitu kizuri kwa taifa kama kuwa na rais mcha Mungu, anayemtanguliza Mungu wetu mbele katika kila kitu, jambo hili limenifurahisha sana na nimeliunga mkono.
Kama kuna kitu hunifurahisha kwa rais wangu ni ucha Mungu wake, siku zote hawezi kumaliza hotuba bila kusema “Tumtangulize Mungu mbele,” anaamini katika Mungu na anataka taifa lake liwe ni la watu wanaomcha Mungu; aliuita ugonjwa wa Corona kama Ka-corona kwa sababu anaufahamu uwezo wa Mungu wake, kwamba ugonjwa huu hauwezi kushinda nguvu ya Mungu anayemwabudu.
Watanzania wameitikia wito wa rais wao, watu wa imani mbalimbali wakapiga magoti na kusujudu mbele ya Mungu wao wakimlilia aiepushe nchi yetu na baa hili, naamini Mungu amesikia na majibu tutayapata hivi karibuni, ndani ya nafsi yangu nasikia kabisa kitu kinaniambia “Ugonjwa huo wa Corona hautavuka Mei 20, 2020”.
Lakini pamoja na wito huu wa rais ningependa kuongezea kidogo tu ya kwamba nyuma ya imani yetu hii, yatupasa tuweke matendo maana kama nilivyosema hapo juu imani bila matendo imekufa! Ni bure.
Ninaposema matendo hapa ninamaanisha nini? Kamwe hatuwezi kupuuza mambo ambayo wataalam wametueleza; kunawa mikono na maji tiririka pamoja na sabuni, kubakia nyumbani, kuvaa barakoa, kujiepusha na mikusanyiko, kujitenga pale unapobaini kwamba una maambukizi na kuwahi hospitali mapema ili kuwaokoa wengine.
Kusali kumwomba Mungu kwa siku tatu wakati huvai barakoa, unashiriki kwenye mikusanyiko, hunawi mikono kwa maji tiririka na sabuni itakuwa ni matumizi mabaya ya imani zetu, ni sawa na yule bwana aliyefunga kwa siku tatu ili taa ndani ya nyumba yake izime, haikuzima lakini akaja mtu asiye na imani akazima swichi na mwanga ukaondoka.
Pamoja na kuendelea kusali tukimwomba Mungu wetu, yatupasa tuendelee kwa juhudi kubwa kutekeleza maelekezo ya wataalam ambao Mungu aliwapa akili, hekima na maarifa wakagundua mambo ya kufanya ili sisi tuepuke kifo. Kuyakataa haya tutaangamia hata kama tumesali kwa siku tatu maana imeandikwa katika Hosea 4:16 ya kwamba “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa…”
Maarifa tumepewa, basi inatupasa juu ya kusali kwetu, tuyatumie, kwani hayo pamoja na sala zetu ndiyo yatakayotuepusha na mauti. Kuendelea tu kusali kwa imani bila kuweka matendo nyuma ya imani zetu hakutatusaidia chochote, matendo yaambatane na sala zetu hapo ndipo tutakapokikwepa kifo.
Tofauti na hapo maambukizi na vifo vitazidi kuongezeka na imani yetu itaonekana haina maana kwa sababu tu tulishindwa kuweka matendo nyuma yake.
Nawafurahia sana viongozi wa dini wanaowaambia waumini wao kwamba “Salini lakini pia fuateni masharti na maelekezo ya wataalam” lakini nachukizwa mno na watumishi wa Mungu wanaowajaza waumini wao kwenye makanisa wakati wanaelewa kabisa kufanya hivyo kutawaletea maambukizi na hatimaye kifo, huku ni kumjaribu Mungu.
Mungu ibariki Afrika,
Mungu ibariki Tanzania,
Mungu mbariki Rais wetu,
Mungu tubariki Watanzania na utuepushe na janga hili.
Ahsanteni kwa kunisoma.
