×

HATARI! Vifaa Vya Hospitali Vyazagaa Mtaani

WANANCHI wa Mtaa wa Makongoro uliopo katikati ya Mji wa Morogoro wako hatarini baada ya vifaa vya hospitali vilivyotumika kuzagaa mtaani kwao.

Kuzagaa huko kunatokana na wasiojulikana kuugeuza mtaa huo kuwa dampo la kutupia vifaa hivyo zikiwemo sindano zilizotumika, mikasi, nyembe na chupa za dawa.

 

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Makongoro, Salama Chika amethibitisha kuwepo kwa dampo hilo la vifaa vya hosptali na kushangazwa nalo.

“Katika mtaa wangu kuna hospitali kubwa mbili, Ahmadya na St. Harry, sasa sijui ni hospitali ipi kati ya hizi inahusika na uchafu huu hatari.

 

“Nilipopewa taarifa hii nilifika kujionea jambo hili hatari kwa afya zetu na hasa watoto ambao hupenda kuokota vitu hovyo.

“Nimeshangazwa kwa kweli, nimepekua sana mabaki haya ya takataka ili nijue yametoka kwenye hospitali gani ili nichukue hatua, lakini nimekosa ushahidi,” alisema mwenyekiti huyo ambaye anaonekana ukurasa wa nyuma wa gazeti hili akiwa kwenye dampo hilo.

Aliongeza kuwa, kabla ya tukio hilo, awali kulikuwa na watu ambao waligeuza mtaa huo kuwa dampo, jambo ambalo lilimfanya aweke watu wa kulinda eneo hilo ili kuwatia nguvuni.

Baada ya mwandishi wetu kutajiwa hospitali ambazo zinatuhumiwa kutupa taka hizo, alifunga safari kwa lengo la kutaka kujua ukweli wa jambo hilo.

 

Kwa kuanzia, mwandishi wetu alifika kwenye Hospitali ya Ahmadya na kukutana na Linna Mamiro ambaye ni katibu wa hospitali hiyo na kumuuliza endapo hospitali yao inahusika na uchafuzi huo wa mtaa.

 

“Sisi tuna ushirikiano na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na taka zetu tunazipeleka kule na zinachomwa moto kwa dawa maalum.

“Kama unavyojua mabomba ya sindano hayawezi kuungua kwa moto wa kawaida, labda vifaa hivyo vimetupwa na hao jirani zetu, nendeni mkawaulize,” alisema Linna.

 

Baada ya majibu hayo, mwandishi wetu alitinga kwenye Hospitali St. Harry iliyopo jengo la tatu kutoka Hospitali ya Ahmadya inayomilikiwa na Watanzania wenye asili ya Asia kwa lengo la kutaka kujua kama ni wao wanaohusika na utupaji huo wa taka hatari au la!

 

Kwa sharti la kutotajwa majina yao, baadhi ya manesi wa hosptali hiyo walisema wao hawahusiki huku nao wakiwatuhumu jirani zao kwamba huenda ndiyo wanaohusika.

“Hospitali yenye wateja wengi ni hiyo ya wenzetu na huo mzigo wa sindano uliotupwa hapo huoni kwamba wao ndiyo wa kuulizwa?

 

“Sisi wateja wetu ni wachache hatuwezi kuwa na shehena kubwa namna hiyo ya mabomba ya sindano yaliyotumika,” alisema mmoja wa manesi hao na kuongeza kuwa, wahusika wakuu wa hospitali hiyo ambao wangeweza kutajwa majina yao gazetini wako safarini.

 

Hii ni mara ya pili kwa mwandishi wetu kujionea dampo kama hilo la taka hatari ambapo awali gazeti ndugu na hili la Uwazi, liliwahi kuandika habari zinazohusu wasiojulikana kutupa taka hatarishi kwenye mtaa huo na hatua stahiki kuchukuliwa na mamlaka husika.

STORI | Dustan Shekidele, Risasi

Leave a Comment