UONGOZI wa Azam FC umesema kuwa tayari ukarabati wa Uwanja wa Azam Complex umekamilika asilimia zote ukiwa sawa na ule wa TP Mazembe.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Ofisa Habari wa Azam FC, Zaka Zakazi alisema kuwa ubora wa uwanja huo kwa sasa ni wa kimataifa.
“Uwanja wetu ubora wake upo sawa na ule Uwanja wa TP Mazembe ya Congo kwa sababu nyasi zake ni 3G, yaani Third Generation ya Artificial (toleo la tatu) turf hili ndilo toleo jipya la nyasi za bandia, 4G bado ila ule wa zamani ulikuwa ni 2G, kama wa Uhuru, Kaitaba, Karume na Simba.
“Hata muundo wa magoli pia ni wa kisasa tofauti na magoli yale ya zamani yaani hapa ni burudani tu mchezaji anaweza kujigonga asihisi maumivu makubwa kwani magoli siyo ya chuma ni ya kisasa kabisa, kinachosubiriwa ni shughuli za michezo kurejea mambo yaanze,” alisema.
Kwa sasa Ligi Kuu Bara imesimamishwa Azam FC walikuwa wanatumia Uwanja wa Uhuru na Taifa kwa mechi zao za nyumbani
Stori na Lunyamadzo Mlyuka,
