×

Wakili Msando Aachiwa kwa Dhamana, Gwandu Aitwa Polisi

WAKILI maarufu Albert Msando hatimaye ameachiwa huru kwa dhamana  baada ya kushikiliwa na polisi jijjni Arusha na kuhojiwa kwa saa kadhaa tangu juzi.

 

Kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoani humo, Moita Koka, amesema wakili huyo ameshikiliwa kutokana na video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii inayoonyesha  mtuhumiwa akieleza kwamba hali ni mbaya sana Arusha kuhusiana na ugonjwa wa homa ya Covid-19 unaotokiana na virusi vya corona wakati hana mamlaka ya kueleza lolote juu ya ugonjwa huo.

’’Ukweli ni kwamba na ninasema bila kuficha hali ni mbaya kwa Arusha ndugu waandishi nyinyi lazima mfike mahali muweke miguu chini mseme ukweli ili wananchi, serikali na kila anayehusika atambue kwamba tupo katika hali mbaya ambayo kila mmoja wetu anapaswa kuchukua hatua mkirudi nyuma na kuogopa kusema tutazikana.

 

Kamanda Koka, amesema kuwa mtuhumiwa alitoa kauli hiyo April 27, 2020,  wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati akigawa vifaa vya kujikinga na virusi vya Corona eneo la Kaloleni katika ofisi ya chama cha waandishi habari mkoa wa Arusha.

 

Aidha ikumbukwe kwamba serikali ilitoa maelekezo kuwa wenye mamlaka ya kutoa taarifa juu ya ugonjwa huo ni waziri mkuu ,waziri wa afya,  maendeleo ya jamii,  jinsia na watoto au mganga mkuu wa serikali.

 

Katika tukio jingine jeshi la polisi linamshikilia Agnes Ndimu Shinji (49) Mkazi wa Lemara jijini Arusha kwa tuhuma za kusambaza taarifa za uongo mtandaoni.

 

Amesema mnamo Aprili 9, 2020, mwaka huu mtuhumiwa kupitia group la Whatsap liitwalo Football for Life, alituma taarifa kwamba mtangazaji wa TBC1, aitwaye Gloria Maiko, amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa corona, kitu ambacho si kweli na hali iliyozua taharuki kwa ndugu na jamaa.

 

Amesema kuwa mara baada ya  polisi kubaini uzushi wa taarifa hiyo,  ilianza kumfuatilia na April 29, 2020,  ilimkamata ambapo katika mahojiano alikubali kulifahamu tukio hilo la kutuma taarifa ya kifo cha mtangazaji huyo bila kuwa na uhakika.

 

Aidha Koka, amesema anatoa onyo kwa viongozi wa siasa pamoja na wananchi kwa ujumla kutokuwa wasemaji wa serikali na wanapaswa kutii amri na maelekezo yanayotolewa na viongozi wakuu wa serikali badala ya kwenda kinyume kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na wale watakaofanya hivyo watakamatwa.

 

Hata hivyo,   Msando ameachiwa kwa dhamana  leo baada ya kulala mahabusu na yupo huru na kutakiwa kuripoti hapo kesho.

 

Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari Arusha (APC), Claud Gwandu, ameitwa polisi kutoa maelezo kuhusu tuhuma za wakili Albert Msando kutoa kauli za uchochezi kuhusu ugonjwa wa corona.

Leave a Comment