WAKATI maambukizi ya Virusi vya Corona yakiendelea kuitesa dunia, wachezaji wa Simba wamepewa onyo kali na kutakiwa kuwa makini kwa kuchukua tahadhari zote za kujikinga na maambukizi hayo yanayosababisha Ugonjwa wa Covid-19.
Hatua hiyo imekuja hivi karibuni baada ya uongozi wa timu hiyo kugundua kuwa kuna baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wanauchukulia kawaida ugonjwa huo na hawachukui tahadhari zote za kujikinga.
Akizungumza na Championi Jumamosi, kiungo mkabaji wa timu hiyo, Jonas Mkude alisema kuwa hali hiyo imemfanya daktari wa klabu hiyo, Yassin Gembe kuchukua uamuzi huo wa kuwataka kuwa makini na kuchukua tahadhari zote za kujikinga na Corona.
“Tupo tunaendelea na harakati za kuhakikisha tunakabiliana na Corona lakini pia wakati huo kila mtu anaendelea kujifua vilivyo peke yake ili kuhakikisha anaendelea kuwa fiti katika kipindi hiki ambacho ligi zimesimama.
“Hata hivyo, tumepigwa mkwara na uongozi juu ya kuchukua tahadhari zote za kujikinga na Corona sababu inasemekana kuna baadhi yetu hawapo makini.
“Kwa hiyo, daktari wetu, Gembe ametutaka kuhakikisha tunakuwa makini na ugonjwa huu,” alisema Mkude.
Stori: Sweetbert Lukonge, Championi Jumamosi
