“SISI wachunga ng’ombe, nafahamu hata mzee wetu Kikwete (Jakaya), kwa sababu ana ng’ombe. Ng’ombe akikatika mkia, humzuii kuingia zizini, japo wenzake watajua huyo hana mkia.”
Hiyo ni kauli ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais John Magufuli ambayo aliitoa Julai 23 mwaka 2016 wakati wa mkutano mkuu wa kukabidhiwa kijiti cha uenyekiti kutoka kwa mtangulizi wake, Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.
Kauli hiyo ya Rais Magufuli, iliibua mijadala huku wengine wakitafsiri kwamba, mwanachama akishahama CCM, anakuwa ameshapoteza sifa ya kuwa mwanachama na anakuwa tofauti na wenzake anaowakuta pale anaporejea.
Lakini wengine wakaenda mbali zaidi na kutafsiri kuwa, wanaorejea CCM kutoka upinzani baada ya kuhama chama hicho katika kipindi cha uchaguzi, hawapaswi kubaguliwa kwa kuwa wamerejea nyumbani ingawa pia watakuwa na alama ya kuwa, waliwahi kukihama chama hicho.
Kiujumla waliokatwa mikia ndani ya CCM ni wengi, hii ina maanisha kuwa wengi wao wamesharejea ndani ya CCM kutokana na vuguvugu la uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Uchaguzi huo ambao uliacha majeraha kwa CCM na kutoa faida kwa upinzani ambapo walifanikiwa kupata kura zaidi ya milioni sita, na wabunge wengi wa upinzani, jambo ambalo halijawahi kutokea tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Hata hivyo, CCM imetumia kila mbinu kuwarejesha waliokatwa mikia, hakika imefanikiwa katika hilo, haijalishi wamenunuliwa, wameshawishiwa, wameahidiwa vyeo ama lah, cha msingi waliokatwa mikia wamerejea, tena amerejea hadi kiongozi mkuu aliyekuwa mgombea urais wa upinzani Edward Lowassa.
Wabunge zaidi ya 10 wamerejea, madiwani na makada mbalimbali kutoka vyama vya upinzani wamerejea CCM, hili ni pigo kwa upinzani hasa Chadema, CUF na ACT Wazalendo.
Tukiweka kando michakato ya CCM, hivi sasa kuna vuguvugu la mpasuko wa upinzani, kwamba vyama vya upinzani vimekumbwa na mpasuko wa aina yake, badala ya wanachama kutoka CCM kuhamia upinzani, wanatoka chama kimoja upinzani na kuhamia chama kingine cha upinzani, hii ina maana kuwa upinzani unanyong’onyezana wenyewe kwa wenyewe, hii si faida kwa uchaguzi mkuu ujao.
Tumeona Chama cha NCCR Mageuzi, namna kinavyokitikisa Chadema, tena kinachoumiza wanachadema zaidi, kimeng’oa makada wa Chadema kwa wingi kuliko wa vyama vingine, hali hii imesababisha sintofahamu kuhusu mustakabali wa NCCR Mageuzi na vyama vyenziye vya upinzani, vilevile utata kuhusu makubaliano ya CCM na NCCR Mageuzi, kwa sababu yapo yanayosemwa kuwa upo uwezekano kwamba huu ni mpango wa CCM kukitumia NCCR Mageuzi kukidhoofisha Chadema.
Ikumbukwe kuwa, Chadema ndicho chama kikuu cha upinzani nchini, kimetumia miaka zaidi ya 18 kujijenga na kuwa na nguvu hiyo, lakini sasa kinaelekea kuporomoshwa katika kipindi cha muda mfupi.
Nasema hivyo kwa sababu wabunge wawili wa Chadema wameshatangaza kurejea NCCR Mageuzi, wabunge hao ni; Anthony Komu (Moshi vijijini) na Joseph Selasini (Rombo), kwa nyakati tofauti wametangaza kurejea katika chama chao cha zamani baada ya kuhitimisha muhula wa ubunge wao mwaka huu.
Ingawa ni pigo kwa Chadema, lakini historia inajirudia, kwa sababu ikumbukwe kuwa makada hao maswahiba, walikuwa NCCR Mageuzi na wameshiriki vuguvugu lote la mageuzi na chama hicho tangu 1992 kabla ya kuhamia Chadema 2009.
Lakini Chadema ndicho chama kilichowaweka zaidi kwenye ramani na kupata umaarufu hasa baada ya kufanikiwa kupata ubunge.
Kilichomuondoa Selasini Chadema ni sababu inayochekesha kama sio kushangaza, kwamba baada ya kuondolewa kwenye kundi sogozi la What’sApp, ndipo alipoamua kujiondoa Chadema kwa sababu kwamba ametengwa, amebaguliwa.
Lakini ikumbukwe kuwa, hili la Selasini ni dhahiri kuwa ni majeraha ya uchaguzi mkuu ndani ya Chadema uliofanyika Desemba mwaka jana, baada ya kuangushwa na Godbless Lema (Mbunge Arusha mjini) katika nafasi ya Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, ndipo hapo mambo yalipoanza kwenda mrama.
Kwa sababu Selasini alijiamini kukamata nafasi hiyo, hasa baada ya kukaimu mwenyekiti wa mkoa na mwenyekiti wa kanda tangu kada maarufu Philemon Ndesamburo kufariki dunia.
Hapo ndipo alipojiuzulu unadhimu kambi ya upinzani bungeni, nafasi aliyokuwa anashikilia baada ya Tundu Lissu kipigwa risasi na watu wasiojulikana 2017. Lakini ndipo Selasini alipoanza kuonesha kuwa vuguvugu yaani, si moto wala baridi, kwa kusifia vilivyo kazi za Serikali na CCM jambo lililokuwa linawakarahisha sana Chadema.
Hadi anatangaza kuhama tayari Chadema wameshamuona si mwenzao, hasa ikizingatiwa komredi wake Komu amerejea nyumbani kwa staili kama ya Selasini.
Kiujumla upinzani wa sasa, unaelekea kuanza kujijenga upya, jambo ambalo si afya kwa ukuaji wa demokrasia nchini, kwa sababu tayari watu waliwekeza Chadema, sasa wamevunjwa moyo, awali waliwekeza CUF, wakavunjwa moyo.
Kwa sababu hiyo tunaiona CUF ikimeguka kuzalisha ACT Wazalendo, huku Chadema nayo ikimeguka na kukiimarisha NCCR Mageuzi.
Je, ni chama gani kingine kinaweza kushika usukani wa kuwa chama kikuu cha upinzani nchini, au Chadema wataweza kuitetea nafasi yao na kuwa na nguvu kama ilivyokuwa 2015?
