×

Nandy: Isingekuwa Corona Ingekuwa Balaa Tupu

DAR: Staa wa Bongo Fleva, Faustina Charles ‘Nandy’ amesema kama siyo janga la Corona angefanya balaa nchini Marekani.

 

Nandy ameliambia Gazeti la IJUMAA WIKIENDA kuwa amelazimika kuahirisha ziara yake ya kimuziki nchini Marekani kutokana na maambukizi ya Virusi vya Corona.

 

Kuahirishwa kwa ziara yake hiyo nchini Marekani kumetokana na athari za Corona ambayo inaitikisa dunia na kusababisha miji mbalimbali kufungwa duniani kutokana maambukizi kuendelea.

 

Nandy alipaswa kuanza ziara yake hiyo Machi 22, mwaka huu ambapo angeanzia Columbus na kuihitimisha Juni 27, mwaka huu jijini Washington nchini Marekani.

 

Pamoja na kuahirisha ziara hiyo Nandy amewajuza mashabiki wake walionunua tiketi kuwa wasiwe na hofu kwani tiketi hizo zitatumika pale watakapotangaza tena kufanyika kwa ziara hiyo.

 

Ugonjwa wa Corona umekuwa na athari kubwa duniani kote hususani nchini Marekani ambapo watu maelfu wanaripotiwa kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo ulioanzia nchini China.

 

Nandy anakuwa mwanamuziki wa pili nchini kuahirisha ziara yake nchini Marekani baada ya Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kufanya hivyo mapema kutokana janga hilo.

Stori: HAPPYNESS MASUNGA, IJUMAA Wikienda

Leave a Comment