


MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini, Slyvestry Koka, amekabidhi Baiskeli 95 zenye thamani ya Shilingi Milioni 25 kwa Viongozi wa Matawi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyopo ndani ya Jimbo hilo kwa ajili ya urahisishaji wa utendaji kazi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya baiskeli hizo kwa viongozi hao wa matawi kwa kata ya Pangani, Maili Moja na Tumbi ambako amemalizia Kugawa Baiskeli Hizo, Mbunge Koka alisema Ameamua kutoa vitendea kazi hivyo ili kurahisisha utendaji kazi kwa viongozi wa Chama hicho kuwafikia wanachama.
“Wakati wa mkutano Mkuu wa CCM wa wilaya niligawa pikipiki 14 kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi wa makatibu Wa kata lakini pia nimeona si vyema nimeamua nikabidhi baiskeli 95 kwa matawi yote yaliyopo ndani ya jimbo la Kibaha Mjini.
Aidha Mbunge Koka ametoa ndoo ya maji, Dawa ya kunawia mikono “Sanitizer” kwa ajili ya kutumika katika Ofisi za Chama za matawi na kata na kuwakumbusha kujihadhari dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona (Covid 19).
Pia Mbunge huyo aamewasisitiza kwa kuwaambia kwa Sasa Bajeti zao zote wazielekeze kununua vifaa vya kujikingia na ugonjwa wa virusi vya Corona (Covid 19) na siyo kununua nguo kwa ajili ya sikukuu na akawasihi wazazi kabla ya kuingia ndani wakitokea kwenye kazi zao wajifukize dawa za miti asili,wabadilishe nguo walizokuja nazo na kuoga maji ya moto.
Aidha Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini, Maulid Bundala alisema kwamba Pikipiki na Baiskeli walizopewa viongozi hao ni vitendea kazi za mali ya Kata na Tawi la Chama Cha Mapinduzi (CCM) isifike mahali wakatumia vitendea kazi hivyo kuwanufaisha katika shughuli zao binafsi watawakwaza wenzao.
Naye Katibu wa CCM Kibaha Mjini, Afidu Luambano amewakumbusha viongozi na wanachama wa chama hicho kwa kuwaambia mwaka huu ni wa Uchaguzi wahimizizane wanachama wa CCM wakajiandikishe na kusahihisha majina yao katika Daftari la kupiga kura kuhakiki majina kama yapo ili wapate ridhaa ya kupiga kura lakini pia wakumbuke kulipia ada ya kadi zao.
NA: ELISA SHUNDA,KIBAHA