×

Ni sahihi wabunge Chadema kujiweka karantini?

GUMZO sasa ndani na nje ya nchi ni Corona ambapo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, wiki iliyopita alisema wabunge wote wa chama hicho kwa wiki mbili hawatahudhuria vikao vya Bunge. Alisema kufanya hivyo ni sehemu ya kujipima kama wameathirika na Corona na kama wameathirika, basi wasiisambaze kwa watu wengine nchini.

Hatua hii ya upinzani inakuja wakati bunge hilo likiomboleza vifo vya wabunge watatu waliofariki dunia katika kipindi cha chini ya wiki mbili.

Gumzo limekolea kwani Chadema kimewataka wabunge wasitishe vikao vya Bunge na kujiweka karantini kwa walau wiki mbili.

Ingawa maofisa wa Bunge hawajahusisha vifo vya wabunge waliokufa na Virusi vya Corona. Serikali imekuwa ikikosolewa kwa madai ya kupuuza janga la Corona na kwa kutoweka hatua kali za kukabiliana na maambukizi ya Corona inayosababisha Ugonjwa wa COVID-19.

Chadema kimekuwa kikisisitiza Serikali iache kupuuza Corona na kuchukua hatua kama zilizochukuliwa na nchi nyingine duniani zikiwemo za Afrika ili kudhibiti maambukizi ya Corona.

Mbowe amekuwa akiishauri Serikali kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na COVID-19.

Uamuzi huo wa Chadema, umeungwa mkono na baadhi ya wanaharakati pamoja na Mbunge wa Kigoma-Mjini kupitia ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, aliyetaka vyama vingine kufuata njia ya Chadema katika kudhibiti ugonjwa huo.

Nilisoma ukurasa wake wa Twitter, Zitto aliandika; “Natoa pongezi za dhati kwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni ndg.@ freemanmbowetz kwa uamuzi huu wa kiuongozi. Hii ni hatua muhimu sana na itachangia kwa kiasi chake kuokoa maisha ya watu. Nawashauri viongozi wengine wa vyama vyenye wabunge kuelekeza wabunge wao kujitenga (isolation).”

Chadema walitoa tangazo lao muda mfupi baada ya kutangazwa kwa kifo cha Balozi Augustine Mahiga ambaye anakuwa mbunge wa tatu kufariki dunia ndani ya siku 11.

Waliomtangulia ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mchungaji Getrude Rwakatare aliyefariki dunia Aprili 20 na Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndasa aliyefariki dunia Aprili 29, mwaka huu.

Licha ya kwamba mamlaka husika hazijatangaza kama wabunge hao walifariki dunia kwa Corona, lakini Mbowe alitoa taarifa kwa umma akisema chama hicho kimeendelea kupokea kwa masikitiko taarifa za misiba ya wabunge na Watanzania wengine inayosababishwa na kusambaa kwa COVID-19.

“Kama ambavyo tumeshauri mara kadhaa, ni dhahiri hatua za ziada za dharura zinapaswa kuchukuliwa kupunguza kasi ya maambukizi na hivyo kuokoa kadiri iwezekanavyo maisha ya Watanzania.

“Wakati tukisubiri wenye mamlaka kuchukua hatua hizo na maadam Chadema tulishasisitiza kila mmoja wetu kuwa mstari wa kwanza wa kujikinga na kukinga wenzake, chama kinatoa maelekezo yafuatayo kwa wabunge wake wote.

“Wabunge wote wa Chadema waache mara moja kuhudhuria vikao vya Bunge au Kamati za Bunge, wabunge wote wa Chadema kutofika kabisa katika eneo lote la Bunge Dodoma na Dar es Salaam, wabunge wote wa Chadema kujiweka karantini kwa muda usiopungua wiki mbili.

“Tunasisitiza wabunge wetu walioko Dodoma wasiende majimboni, mikoani bali wabaki Dodoma kwenye karantini hadi itakapothibitika wao ni salama au kupata maelekezo mengine yoyote yaliyo rasmi,” ilieleza taarifa hiyo.

Lakini pia Chadema imewasihi wabunge wa vyama vingine kutafakari kama ni salama kuendelea na vikao vya Bunge katika mazingira yaliyopo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Chadema walitaka Bunge kusitisha shughuli zake kwa siku 21 ili wabunge na watumishi wa Bunge na familia zao pia wakae karantini, wapimwe ili kubaini ni wangapi wana virusi hivyo ili hatua stahiki za kitabibu zichukuliwe.

Chadema pia walitaka kamati mahususi za Bunge hususan Kamati ya Huduma za Bunge na Kamati ya Uongozi zifanye vikao vyake kwa njia ya mtandao ili maamuzi muhimu kuhusu utawala na mwenendo wa Bunge yaweze kufanyika.

Mahiga ambaye hadi umauti unamfika, alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria, anakuwa ni waziri wa kwanza kufariki dunia tangu Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani Oktoba, 2015 na anakuwa mbunge wa tisa kufariki dunia tangu kuanza kwa Bunge la 11.

Mbali na Balozi Mahiga ambaye ni mbunge wa kuteuliwa na Rais, wengine waliofariki dunia, mbali ya Rwakatare na Ndasa, ni aliyekuwa Mbunge wa Newala-Vijijini (CCM), Rashid Akbar, Stephen Ngonyani (Maji Marefu) aliyekuwa Mbunge wa Korogwe-Vijijini (CCM), Dk Elly Macha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Hafidh Ally Tahir aliyekuwa Mbunge wa Dimani (CCM), Leonidas Gama aliyekuwa Mbunge wa Songea- Mjini (CCM) na Kasuku Bilago aliyekuwa Mbunge wa Buyungu, (Chadema).

Maswali ambayo yanagonga vichwani mwa watu ni kwamba, kwa nini Mbowe ahofie hali ya Corona bungeni? Je, yupo sahihi au amekurupuka?

Kama yupo sahihi, kwa nini Spika Job Ndugai hasikilizi ushauri huo? Je, wakimaliza karantini hiyo na kuonekana wapo salama kama ambavyo alionekana yeye (Mbowe), wataendelea na vikao vya bunge?

Leave a Comment