×

Rekodi Tano Ambazo Hadi sasa Zinaishi

KATIKA soka, kila siku kuna rekodi zinawekwa na zingine kuvunjwa. Wakati huohuo, kuna rekodi ambazo bado ngumu kuvunjwa na zinaendelea kuishi.

Hapa chini kuna rekodi tano ambazo hadi sasa zinaishi.

KUTWAA MATAJI MATANO MFULULULIZO YA UEFA

Mwaka 1956, Real Madrid ilishinda taji la European Cup ambalo kwa sasa linafahamika kama Ligi ya Mabingwa Ulaya. Baada ya hapo ikashinda mfulululizo na kufikia mataji matano.

Mpaka sasa hakuna klabu iliyofanya hivyo. Ajax ilipambana na kushinda mara tatu mfululizo kuanzia 1971 hadi 1973.

Mbali na hilo, pia Real Madrid inashikilia rekodi ya kutwaa mataji 13 ya michuano hiyo.

KUFUNGA MABAO MENGI KOMBE LA DUNIA

Katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1958, Mfaransa, Just Fontaine alifunga mabao 13 katika mechi sita na kuwa mfungaji bora.

Hadi leo hakuna mchezaji aliyeifikia rekodi hiyo katika michuano hiyo.

KOCHA ALIYETWAA MATAJI MENGI

Kocha Alex Ferguson anashikilia rekodi ya kutwaa mataji mengi katika historia ya soka kushinda makocha wengine wote.

Ferguson hadi anastaafu kufundisha mwaka 2013, ametwaa jumla ya mataji 48. Ndani ya Man United pekee ametwaa mataji 38 kuanzia mwaka 1986 hadi 2013.

Miongoni mwa mataji hayo ni Premier League (13), FA (5) na Ligi ya Mabingwa Ulaya (2).

IDADI YA MASHABIKI

Katika fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1950 kwenye Uwanja wa Maracana kati ya wenyeji Brazil dhidi ya Uruguay, mashabiki wengi walijitokeza uwanjani na kuweka rekodi.

Jumla ya watazamaji 173,830 waliingia uwanjani kushuhudia mchezo huo. Hadi leo hakuna uwanja ulioingiza watazamaji wengi kuzidi hao.

KUFUNGA MABAO MENGI MSIMU MMOJA

Mwaka 2012, Lionel Messi aliweka rekodi ya kipekee katika ufungaji baada ya kumaliza akiwa na mabao 91.

Messi alifunga mabao 59 katika mechi 38 za La Liga, Copa del Rey (5), Ligi ya Mabingwa Ulaya (13) na Supercopa (2). Upande wa timu ya taifa ya Argentina alifunga mabao 12 katika mechi 9.

Kwa jumla, Messi alicheza mechi 69 na kufunga mabao 91. Akavunja rekodi ya Gerd Muller aliyefunga mabao 85.

BARCELONA, HISPANIA

Leave a Comment