×

Lockdown Suluhu Ya Mapambano Dhidi Ya Corona?

WAKATImaambukizi ya virusi vya Corona yakitimiza miezi mitano tangu mlipuko wake ulipoanza Disemba mwaka jana nchini China, nchi mbalimbali zimechukua hatua kadhaa katika kujihami dhidi ya virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

 

Hadi sasa virusi hivyo vya Corona vimesababisha vifo zaidi ya 280,000 duniani, huku watu zaidi ya milioni 4.2 wakiambukizwa. Kwa upande wa Tanzania hadi Mei 12 mwaka huu, watu 480 walikuwa wameambukizwa huku vifo 16 vikitangazwa na Serikali kutokana na ugonjwa huo.

 

Mlipuko wa virusi hivyo ulioanzia katika mji wa Wuhan nchini China, na kuenea katika nchi zaidi ya 210 duniani, asilimia 90 ya nchi hizo ziliangukia katika kundi la kuzuia raia wake kutoka nje (lockdown), na kufunga shughuli zote za kijamii ikiwamo mikusanyiko ya aina mbalimbali.

Nchi hizo zikiongozwa na China, Marekani, Italia, Uingereza na nchi nyingine za Ulaya, Asia na Afrika, ‘zilicopy’ na ‘kupaste’ mfumo huo wa lockdown ili kunusuru maambukizi ya Corona yasisambae kwa kasi kwa wananchi wake.

 

Hata hivyo, upande wa Tanzania hali ilikuwa ni tofauti, kwani badala ya kuiga mfumo wa lockdown kama zilivyofanya nchi za Kenya, Rwanda na Uganda, Tanzania ilizuia baadhi ya shughuli kama vile kufunga shule, vyuo, kuzuia mikusanyiko isiyo ya lazima huku baadhi ya shughuli zikiendelea kama kawaida.

 

Wakati Rais John Magufuli akiendelea kutetea uamuzi huo, na kubainisha sababu za msingi ikiwamo jiji la Dar es Salaam kuwa kitovu cha uingizaji na upitishaji wa bidhaa kuelekea nchi jirani zisizo na bandari, baadhi ya Watanzania na mashirika ya kimataifa yalipinga vikali uamuzi huo na kumtafsiri rais kama mtu asiyejali uhai wa wananchi wake, kumbe la hasha!

 

Hali imekuwa tofauti, kwani katika nchi ambazo ziliongoza kwa mbinu hizo za lockdown, sasa zinajutia uamuzi huo huku zikianza kulegeza masharti kidogokidogo baada ya kubaini, kuzuia wananchi kutoka nje sio suluhu pekee ya kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.

Maeneo ya Ulaya yameanza mchakato wa kufungua upya nchi zao baada ya kufungwa kutokana na virusi vya Corona. Hali hiyo inaonesha jinsi serikali zinavyokabiliwa na hali ya hatari duniani wakati zikijaribu kufungua uchumi wao wakati huo huo zikijaribu kudhibiti janga hilo.Uingereza sasa inajipanga kulegeza masharti ya ‘lockdown’ kuelekea hali ya kawaida, Ufaransa na Uhispania vilevile zimeingia katika hali ya kulegeza vikwazo.

 

Nchi ya Italia ambayo iliondoa lockdown miezi miwili baada ya kushambuliwa na virusi hivyo vilivyosababisha vifo vya watu zaidi ya 30,000, kuanzia Mei 18 mwaka huu, imelegeza masharti ya kukaa ndani na kuruhusu harusi na ibada kuanza rasmi baada ya makubaliano ya Serikali na viongozi wa dini.AFRIKANchi za Rwanda na Nigeria kuanzia Mei 11 zilianza kulegeza masharti ya amri ya kusalia ndani kwa wananchi wake kama sehemu ya mapambano dhidi ya Corona.

 

Nchini Rwanda marufuku hiyo ilikuwa imewekwa nchi nzima, huku Nigeria marufuku hiyo ikihusisha mji mkuu wa Abuja, na mji mkubwa kabisa wa Lagos, katika jaribio la kupunguza athari ya kiuchumi barani Afrika.Nchi hizo mbili, zinaungana na mataifa mengine ya Afrika kama Ghana, Afrika Kusini na Kenya ambayo pia yamelegeza baadhi ya masharti makali ya hatua hizo za watu kusalia ndani.

 

Mataifa kadhaa ya Afrika yamechukua hatua ya kuweka marufuku hiyo toka mlipuko wa virusi hivyo kuingia barani na kuonesha hatari ya maambukizi ya ndani ya jamii.Uganda pia ilitarajiwa kutangaza kulegeza masharti wiki hii. Raisi Yoweri Museveni alisema baadhi ya shughuli za kibiashara zinatarajiwa kufunguliwa japo shule zinatarajiwa kuendelea kufungwa mpaka hapo itakapotangazwa.

 

Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo tayari ameondoa marufuku ya watu kutoka nje ama ‘lockdown’ katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ambayo yalikuwa yamefungwa ili kudhibiti kusambaa kwa virusi vya Corona.Watu sasa wanatakiwa kuvaa barakoa nchini humo, na makatazo kama kufungwa kwa shule na mikusanyiko ya watu, bado yakiendelea.

 

Mipaka ya nchi hiyo pia itaendelea kufungwa kwa wiki mbili zaidi wakati mapambano dhidi ya virusi vya Corona yakiendelea.Aidha, Waziri wa Afya nchini Kenya, Mutahi Kagwe alitangaza masharti mapya ya uendeshaji migahawa kama njia ya kulegeza masharti ili kufufua uchumi.Migahawa kuanza kufunguliwa kuanzia saa 11 asubuhi hadi saa 10 jioni.Watakaoingia kuhudumiwa watahitajika kufuata utaratibu uliopo wa kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono na kuvaa barakoa kama kawaida.

 

Hatua ya kutokaribiana itaendelea kutekelezwa umbali wa mita moja baina ya mtu mmoja hadi mwingine.Ingawa hatari ya virusi ikiendelea kushamiri, nchi nyingi za Afrika zinalegeza masharti na kuonekana kukabiliana vyema na virusi.

 

Biashara za umma na binafsi pia zimeanza kufunguliwa tena, huku nchi nyingi zikifungua masoko kwa asilimia 50 pekee ya wafanyabiashara kufanya kazi.Mijadala kuhusu lockdown imeendelea kushamiri sehemu mbalimbali duniani, huku swali la msingi likibaki kuwa je, hatua hiyo ya kuzuia watu kutoka nje inasaidia kupunguza maambukizi?

 

Swali hilo linatokana na wasiwasi ulioibuka China licha ya kuwa kuzuia raia wake kutoka nje kwa muda wa zaidi ya miezi miwili, maambukizi ya Corona yameanza tena nchini humo.Wapo baadhi ya marais wanaona sasa hakuna haja ya kufunga miji/nchi (Lockdown), kwani hakuna chanjo au tiba halisi ya Corona, hivyo ni vema jamii yetu ijifunze kuishi na virusi hivi kwa kuchukua tahadhari.

Stori: GABRIEL MUSHI NA MITANDAO

“CORONA ni ya DUNIA Nzima, IMEINGIA hadi IKULU MAREKANI, Nyie Mko BIZE Kuichafua NCHI” – MWIGULU

Leave a Comment